
Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema uchaguzi huo ulenge kuwapata watu sahihi ambao, watakuwa na nia ya kuipeleka Yanga kwenye ushindani wa kimataifa.
“Simba imara inahitaji Yanga imara kwa sababu klabu hizi mbili ni kioo cha soka la Tanzania huo ndio ukweli, uchaguzi utakaofanyika Mei 5 kwa Yanga uwe wa mapinduzi ya kuleta vitu tofauti na vyenye tija sio kama miaka iliopita.
“Natamani ziingie sura mpya na sio wale ambao walikuwepo kwenye uongozi wa nyuma kwani, hawakuweza kufanya kitu chochote.
“Yanga tunahitaji ifike mbali na sio ilivyo kwa sasa mpaka inafikia mahali tunachangishana, klabu hiyo ni tajiri hapa vije vichwa vya kufanya mambo.
“Wanaochagua viongozi waache tamaa za kuchukua posho za wagombea, hilo limewahi kunikuta uchaguzi uliopita niligombea ujumbe watu wanataka niwape pesa natoa wapi sasa. nilipata kura 577, hivyo sikupita kwani walitakiwa 10 tu mimi nilikuwa wa 11.
“Uchumi ndio kikwazo cha wachezaji wa zamani tushindwe kwenda kuchukua fomu ili kusaidia klabu kuwa na soka la mfano, lakini yote kwa yote waje watu makini ambao, wana uwezo wa kubuni mikakati mipya ili kuhakikisha Yanga inafika mbali tofauti na mambo yalivyo sasa”