Ratiba haiwezi kutukosesha ubingwa – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamedhamiria kutetea ubingwa wa ligi kuu walioutwaa msimu uliopita hivyo wako tayari kukabiliana na ratiba ngumu ya viporo waliyopangiwa na Bodi ya Ligi

Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 juzi dhidi ya Coastal Union, kesho Jumamosi Simba itashuka tena uwanjani kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo utakaopigwa dimba la Kaitaba mkoani Kagera

Simba imewasili Bukoba mapema leo tayari kwa mchezo huo

Aussems amekosoa mpangilio wa ratiba ikiwemo kupangiwa kucheza saa nane mchana. Hata hivyo amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari hata wakipangiwa kucheza saa nne asubuhi

“Tumetoka katika kibarua kigumu cha michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumekuja kwenye kazi ngumu ya kutetea ubingwa wetu. Tutakabiliana na ratiba tuliyopangiwa hata tukitakiwa kucheza saa nne asubuhi” amesema

“Kuchukua ubingwa si jambo la kuzungumza kwa mdomo, bali linahitaji matendo yenye uthubutu, ikiwa ni pamoja na mipango yake ndani ya kikosi”

Simba inakabiliwa kucheza michezo minne kanda ya ziwa dhidi ya Kagera Sugar, KMC, Alliance Fc na Biashara United kabla ya kuelekea mkoani Mbeya kuzikabili Tanzania Prisons na Mbeya City