
Uongozi wa Simba umesema mchezo huo ni fursa adimu kwa wachezaji wake kwani utawasaidia kuwajengea uzoefu wa Kimataifa
Aidha Simba imesema itautumia mchezo huo kuitangaza Tanzania Kimataifa kwani wanajua utafuatiliwa na mamilioni ya mashabiki wa soka duniani kwani utarushwa mbashara na runinga mbalimbali kote duniani
Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema uteuzi huo ni sahihi kwa Simba kwani ukiachilia mbali mafanikio waliyopata kwenye michuano ya SportPesa ukilinganisha na timu nyingine za Tanzania, Simba iko kwenye kiwango cha juu zaidi kwa sasa hapa nchini
“Simba kwa sasa ipo katika kiwango cha juu na kucheza na Sevilla kutasaidia kujua viwango vya wachezaji wetu katika mechi za kimataifa,” amesema
“Mechi hii inaiweka Tanzania katika historia kubwa sana katika soka. Historia zinaonyesha kuwa miaka ya nyuma, timu mbalimbali kutoka nje ya mipaka ya Afrika zilikuja hapa Tanzania na kucheza na Yanga na Simba, miaka ya hivi karibuni hakukuwa na ujio huo zaidi ya mwaka 2017 ambapo SportPesa iliileta timu ya Everton na kucheza timu ya Gor Mahia ya Kenya”
Sevilla ni moja ya timu kongwe na maarufu nchini Hispania na barani Ulaya. Imewahi kutwaa taji la Europa kwa misimu mitatu mfululizo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita