MO DEWJI: Apongeza UBINGWA – SIMBA, Aweka wazi Mipango ya Msimu UJAO

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ amewapongeza wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mo amesema ubingwa huo matokeo ya ushirikiano na umoja ulioonyeshwa na Wanamsimbazi tangu mwanzoni mwa msimu

Aidha Mo amesema shamrashamra za ubingwa zitafanyika May 25 wakati timu hiyo itakabidhiwa kombe katika mchezo dhidi ya Biashara United

Katika hatua nyingine Mo ameipongeza Yanga kwa kuipa changamoto Simba katika mbio za kuwania ubingwa.

Amewapongeza viongozi wapya wa timu hiyo na kuwataka waimarishe timu yao ili iweze kuipa changamoto zaidi Simba kwani anaamini uimara wa timu zote utaongeza ubora wa soka la Tanzania

Aussems kuendelea kuinoa Simba

Mo amesema baada ya kocha Mkuu Patrick Aussems kutimiza masharti yote ya mkataba wake, wanakusudia kumpa mkataba mpya

Mwaka jana Aussems aliposaini mkataba wa mwaka mmoja, alipewa masharti mawili ambapo moja ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu na la pili ni kutinga hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Maboresho ya kikosi

Mo amesema Aussems leo atawasilisha ripoti ya maboresho ya Simba kwa ajili ya msimu ujao.

Aussems atapendekeza wachezaji ambao anataka waachwe/watolewe kwa mkopo pia kocha huyo anatakiwa kupendekeza wachezaji ambao anataka wasajiliwe

Mo amesema wamedhamiria kuifanya Simba iwe imara mara dufu ili kuhakikisha inafanya vizuri zaidi kwenye michuano ya CAF msimu ujao

Amesema watashindana na vilabu vikubwa barani Afrika kama Al Ahly, TP Mazembe, Zamalek nk katika kuwania wachezaji wazuri

Kuhusu Kambi

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, Mo amesema msimu huu Simba itaweka kambi barani Ulaya katika nchi ya Ureno au nchini Marekani

Leave a comment