RATIBA ya KLABU BINGWA AFRICA

Droo ya ratiba ya awali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu wa 2018/19 ilifanyika nchini Morocco Novemba 03, 2018 lakini haikuwa imetangazwa rasmi na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.

Ratiba hiyo imetangazwa rasmi leo ambapo Simba sasa itachuana na Mbabane Swallows, mabingwa wa ligi kuu ya Swaziland.

Taarifa za awali kuwa Simba ingechuana na timu ya Ngozi inayomilikiwa na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza hazikuwa sahihi na zilitokana na mkanganyiko wa ratiba hiyo

Mchezo wa kwanza utapigwa kwenye uwanja wa Taifa mwishoni mwa mwezi huu Novemba 27-28 huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa nchini Swaziland Disemba 04-05.

Mbabane Swallows sio timu ya kubeza. Timu hiyo ndiyo aliyotokea Asante Kwasi kabla ya kuja nchini na kiungo wa Yanga Papi Tshishimbi.

Misimu miwili iliyopita Swallows iliiondosha Azam Fc kwenye raundi ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho na yenyewe ikafanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Aidha timu hiyo msimu uliopita ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa ikipangwa kundi moja na Etoile Du Sahel, Zesco United na 1st De Agosto

Ilimaliza nafasi ya mwisho ikiwa na alama nne katika kundi D ambalo timu ya 1st De Agosto ilifanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano hiyo inayofikia tamati leo kwa mchezo wa marudiano wa fainali kati ya Esperance dhidi ya Al Ahly ambayo ilishinda kwa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita

Wawakilishi wengine wa Tanzania, kutoka upande wa Zanzibar, JKU wao wataanzia ugenini katika mchezo dhidi ya Al Hilal ya Sudan

Kama Simba itafuzu hatua ya awali, raundi ya kwanza ikachuana na mshindi kati ya UD Songo ya Msumbiji dhidi ya Nkana Fc ya Zambia

Leave a comment