Achana na shangwe la wachezaji wa Yanga baada ya kusikia Mwenyekiti wao, Yusuf Manji amerejea katika nafasi yake, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mwinyi Zahera ghafla tu amefunguka akisema taarifa hizo zilizomshtua kisha akasema, kama mkubwa amerudi basi ubingwa Yanga ni mali yao.
Pia, Zahera amesema mkakati wake wa kusajili mastaa watatu wa maana ndani ya kikosi chake, umepata mzuka kwani, anaamini mabosi wa Kamati ya Usajili ikiongozwa na Hussen Nyika, watamkabidhi majina hayo.
Akizungumza na Mwanaspotikutoka kwao DR Congo Zahera amesema kurejea kwa Manji na kama mambo yatatulia baada ya kurudi kwake, basi Yanga haiwezi kupishana na ubingwa msimu huu.
Alisema kila walipokuwa wakikutana na wakati mgumu katika timu yao walikuwa wanakumbushana kumwombea Manji ili mambo yakae sawa na arejee ili arudi klabuni.
Kocha huyo alisema kurejea kwa Manji kisha Yanga ikafanya usajili aliokusudia kuufanya, hakuna namna timu yake inaweza kuukosa ubingwa msimu huu.
Amesisitiza kuwa akirejea ataliamsha kwa wachezaji wake kwa kuwataka kufanya kazi kwa nguvu zaidi kwani sasa matatizo yao yatashughulikiwa na uongozi na wao wanatakiwa kuchapa kazi.
“Nimeshtuka sana kusikia hizo taarifa, niliacha hata kula, nimefurahi sana hii ni habari njema kwangu na kwa Wanayanga wote wanaotaka mafanikio ya hii timu,” alisema Zahera.
“Hamjui kila wakati tulikuwa tunaambiana kwenye timu tuzidishe maombi tumwombee kiongozi wetu Manji arudi kila mchezaji na wasaidizi wangu wanajua nguvu ya bosi wetu.
“Nasema kama Manji amerudi halafu tukafanya usajili wa wachezaji watatu ambao, nataka kufanya kwenye dirisha dogo, sioni nani anaweza kuizuia Yanga isiwe bingwa.
“Tusubiri kuona lakini nikirudi wachezaji wangu wajiandae nataka tufanye kazi ya nguvu kuliko iliyofanyika nyuma ili tumrudishe kwa mafanikio kiongozi wetu, najua matatizo yao sasa yatashughulikiwa.
Wachezaji nao walipuka
Kule nchini Afrika Kusini walipo baadhi ya wachezaji wa Yanga katika kambi ya kikosi cha Taifa Stars ongeza na wale waliobaki nchini wamelipuka kwa furaha wakisema ‘bosi karudi’.
Kiungo Feisal Salum “Fei Toto alisema bado haamini licha ya kuona vipande vya video na picha juu ya kurejea kwa Manji.
“Mpaka sasa siamini hizo taarifa naona picha na video lakini nikimwona nitaamini zaidi hii ni habari njema kwetu,” alisema Fei Toto.
Naye beki Andrew Vincent “Dante alisema wamepokea kwa faraja taarifa hizo na sasa wanasubiri kutangaziwa rasmi na viongozi wao.
“Kusema kweli hakuna ambaye anaweza kusikia taarifa za Manji karudi alafu akanuna labda awe sio mtu anayetaka mafanikio ngoja tusubiri viongozi waje watutangazie kwanza,” alisema Dante