Kiraka wa kimataifa na beki tegemeo wa Simba, Shomary Kapombe ameendelea na mkosi wa kuumia akiwa na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ baada ya kupata majeraha yakayomweka nje ya uwanja wa muda mrefu.
Kuumia kwa Shomary, kumemtibua Kocha Mkuu wa Simba na mabosi wa klabu hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Wekundu wa Msimbazi wanakabiliwa na mechi ngumu kwa sasa, hivyo kuilazimisha Simba isake mbadala yake bila matarajio.
Kocha Aussems alisema kuumia kwa Kapombe ni pigo kwa kikosi chake na anawasiliana na viongozi kuona wanafanya nini katika dirisha dogo ili kuziba nafasi yake, ingawa anakiri mbadala wake hatamtumia mechi za CAF.
Beki huyo wa pembeni anayemudu beki ya kati na kiungo, aliumia pia mwaka jana akiwa na Stars katika michuano ya Cosafa na majeraha yake yalimweka nje ya uwanja kwa muda mrefu wakati huo akitua Msimbazi kutoka Azam FC.
Majeraha ya awali yalimfanya Kapombe alijigharamie kujitibu mwenyewe Afrika Kusini na hata sasa akiumia akiwa Lesotho kumembakisha Afrika Kusini na taarifa zinasema atakuwa nje kwa muda wa miezi miwili kutibu jeraha la kifundo cha mguu.
Hata hivyo, kwa sasa Simba imebeba jukumu la kumtibu mchezaji huyo tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Mbelgiji, Patrick Aussems, ili kuhakikisha anarudi uwanjani haraka.
Jeraha hilo limewatia hofu viongozi wa Simba ambao wanajiandaa na mechi ya kwanza ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland kati ya Novemba 27 na 29 itakayochezwa jijini Dar es Salaam.
Aussems sasa atalazimika kuwatumia wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho ambapo nafasi ya Kapombe ndani ya Simba anayeweza kumudu kuicheza ni Erasto Nyoni kwani Nicholous Gyan hata kama anaweza ila jina lake halijapelekwa CAF kwa ajili ya michuano hiyo.
Kwenye michuano ya ligi, Aussems huenda akasajili beki mpya atakayeendana na kasi ya Kapombe ili pengo lisiwepo hata kama atalazimika kuendelea kumtumia Nyoni basi nafasi ya beki, lakini lazima asajili kama atahitaji kuongeza nguvu ingawa yupo Juuko Murshid na Pascal Wawa.
Tetesi zilizopo ni kwamba beki wa Prisons, Salum Kimenya yupo mawindoni ingawa imeleezwa kwamba hata wakimnasa beki huyo basi itakuwa ni kwa ajili ya ligi na sio michuano ya kimataifa.
Kocha mchambuzi wa soka, Dk Mshindo Msolla alifafanua hilo, “Kimenya ni mzuri lakini kwa Simba hii bado sana, hawezi kuvaa viatu vya Kapombe hata siku moja, ni mzuri kwa timu nyingine kama wanatafuta mrithi wa Kapombe kwa kipindi hiki basi waende nje ya nchi kwa hapa Tanzania hakuna zaidi ya Erasto Nyoni ambaye pia hamudu vyema.
“Kapombe atabaki kuwa Kapombe kwenye ligi hii, kocha akimtoa Nyoni kucheza pale kati basi asajili beki mwingine wa katikati na si vinginevyo,” alisema Msolla Kauli hiyo iliungwa na Joseph Kanakamfumu kwamba Kimenya si mchezaji wa kucheza Simba hii yenye kusaka mafanikio makubwa na imepiga hatua ndefu.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ alielezea hali ya Kapombe huko Afrika Kusini kwamba;
“Anaendelea vizuri na atakuwa nje kwa miezi miwili, ni pigo kwetu na sasa tunamshughulikia ili apone haraka na kurejea kwenye majukumu yake, mapendekezo yatakayoletwa na kocha kuhusu nafasi yake yatashughulikiwa haraka”.