Uongozi wa Yanga umeliomba Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liingilie kati kumaliza mvutano uliopo kati ya TFF na Yanga kuhusu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi utakaofanyika Januari 13 2019.
Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi zilizotangazwa lilifungwa rasmi jana Jumatatu saa 10:00 jioni lakini uongozi wa Yanga umeendelea na msimamo wake wa kupinga uchaguzi kwa nafasi ya Mwenyekiti.
Yanga pia haikubaliani na uchaguzi wake kusimamiwa na TFF.
Taarifa iliyopatikana jana ilieleza kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameunga mkono uamuzi wa Yanga kwenda BMT kusaka suluhu kwani anaamini Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga anaweza kumaliza utata huo.
“Nimesikia upande mmoja unataka kwenda BMT nimefurahi sana waende wakae chini ya mwanasoka mzoefu Tenga (Leodegar) awasikilize pande zote mbili kuna shida gani ikishindikana pale litakuja kwangu,”Dk Mwakyembe amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti.
“Mimi naamini hili ni suala la kutumia busara tu, sioni kama ni gumu halina ugumu wowote wanachoshindana ni mambo mawili kwanza wanataka kamati yao ya uchaguzi ndio isimamie uchaguzi na TFF wanasema mbona hamtoshi, ni mvutano huo sasa tutaangalia kama wanaweza au kama hawawezi tutafanya maamuzi.
“Pili ni kuhusu Yusuf Manji hakuna anayekataa kwamba Wanayanga wanampenda sana, lakini katika nchi kuna kanuni na sheria hata kama unampenda, we mpende nyumbani kwako unapokuwa kwenye nchi kuna sheria, lazima tuangalie kuna kitu gani Yanga wanataka na sheria pia,” aliongeza Dk Mwakyembe
Pia wakati Yanga ilipokwenda Ruangwa kucheza na Namungo kwenye mchezo wa kirafiki, viongozi wa timu hiyo walimuomba Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo kuingilia kati kupata suluhu ya mgogoro huo