Full Time : Yanga 2-1 Biashara United

Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Yanga wameendeleza ubabe kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuilaza Biashara United mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa leo.

Huo ulikuwa ushindi wa 13 kwa Yanga katika michezo 15 waliyocheza, wakitoka sare michezo miwili tu

Biashara United iliandika bao la kuongoza kwenye dakika ya 38 baada ya kufanya shambulizi la kushitukiza lililomaliziwa vyema na Mangalo

Yanga imedhihirisha kuwa ni timu isiyofungika kwa urahisi kwani katika kipindi cha pili ilipeleka mashambulizi mengi langoni kwa Biashara United waliokuwa wakicheza kwa kujihami

Bao la kusawazisha la Yanga liliwekwa kambani na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwenye mchezo wa leo kocha Mwinyi Zahera alimchezesha kama kiungo

Shaibu alimalizia vyema pasi murua ya Amisi Tambwe aliyeingia katika kipindi cha pili.

Aliyeipa Yanga matokeo muhimu sio mwingine zaidi ya Heritier Makambo aliyefunga bao safi kwenye dakika ya 80 na kuihakikishia Yanga alama tatu muhimu

Makambo aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi uliopita, amefikisha mabao nane sasa akiwa nyuma ya Eliud Ambokile wa Mbeya City kwa tofaurti ya bao moja tu.

Yanga imerudi kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 41, alama mbili zaidi ya Azam Fc iliyo nafasi ya pili

Aidha matokeo hayo yanaifanya Yanga izidi kuitimulia vumbi Simba sasa ikiachwa kwa tofauti ya alama 14 licha ya kuwa na michezo mitatu ya kiporo