Wekundu wa Msimbazi, Simba wametinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa staili ya aina yake baada ya kuifumua Nkana Fc mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa leo.

Bao la kideo lililoipeleka Simba hatua ya makundi liliwekwa kimiani na kiungo fundi, Clatous Chama kwenye dakika ya 88 akimalizia pasi ya Hassani Dilunga ‘HD’.

Nkana Fc hawatalisahau bao hilo na hakika Wazambia hao hawatamsahau ‘ndugu yao’ Chama kwani leo alikuwa kama hawajui.

Ilikuwa ni Nkana Fc iliyotangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Walter Bwalya kwenye dakika ya 17. Bao hilo liliiharibia Simba hesabu kwani awali ilikuwa ikihitaji ushindi wa bao 1-0.

Licha ya kuwa nyuma kwa bao la mapema, mabingwa hao wa Tanzania Bara hawakukata tamaa na walifanikiwa kusawazisha kwenye dakika ya 30 kupitia kwa shuti la Jonas Mkude aliyemalizia pasi ya Chama.

Meddie Kagere akaiongezea Simba bao la pili kwa kichwa dakika chache kabla ya kwenda mapumziko kabla Chama hajafunga bao la ‘usiku’ lililoipeleka Simba hatua ya makundi.

Matokeo hayo ni ushindi mwingine wa kihistoria kwa Simba ambayo sasa imerejea hatua ya makundi baada ya kusubiri ka miaka 15.