
Wakicheza kandanda safi na ya kuvutia vijana wa Aussems waliwapoteza kabisa Saoura waliojikuta muda mwingi wakiusaka mpira ‘kwa tochi’
Simba ilifanya mashambulizi mengi langoni kwa Saoura kwenye kipindi cha kwanza Mganda Emmanuel Okwi akikosa nafasi mbili mapema kabisa
Baada ya kosakosa nyingi, Okwi alisahihisha makosa yake na kuiandikia Simba bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Clatous Chama, Okwi aliwahadaa walinzi wa Saoura kabla ya kuujaza mpira kimiani.

Mabadiliko yaliofanywa na Aussems kwenye dakika ya 35 kwa kumuingiza Meddie Kagere kuchukua nafasi ya Bocco aliyeumia, yalikuwa na faida kwa Simba kwani alikuwa ni Kagere aliyeiongezea Simba mabao mawili katika kipindi cha pili.
Kagere aliifungia Simba bao la pili kwenye dakika ya 52 akimalizia pasi murua ya Okwi aliyevunja mtego wa kuotea.
Katika dakika ya 62 Okwi tena akamuwekea Kagere pasi mpenyezo na bila ajizi Kagere akaweka bao la tatu kimiani.
Ushindi huo ni matokeo stahili kwa Simba kutokana na ubora walioonyesha katika mchezo wa leo.
Simba inaongoza kundi D ikiwa na alama tatu na mabao matatu. AS Vital na Al Ahly vitachuana leo katika mchezo mwingine wa kundi D
Wiki ijayo Simba itasafiri kwenda nchini Congo kuivaa AS Vital katika mchezo mwingine wa raundi ya pili