Alikufa Al Ahly uwanja Taifa, Vita ni nani

Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya JS Saoura Jumamosi iliyopita kwa kufungwa mabao 2-0, Jumamosi ijayo Simba inarejea kwenye uwanja wa Taifa kumaliza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwa kuikabili AS Vita Club

Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote kwenye mchezo huo ili iweze kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili katika historia yake

Simba iliwahi kutinga robo fainali ya michuano hiyo mwaka 1974

Kwenye msimamo wa kundi D JS Saoura inaongoza ikiwa imejikusanyia alama nane ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama saba sawa na Vita Club ambayo inashika nafasi ya tatu

Simba inashika nafasi ya nne ikiwa na alama sita

Bila ya kujali matokeo kati ya Al Ahly dhidi ya JS Saoura, ushindi utaihakikishia Simba kufikisha alama tisa na kujihakikishia moja ya tiketi mbili za kutinga robo fainali

Habari njema kwa Simba ni kwamba itakuwa ikicheza mchezo huo mbele ya mashabiki wake ambapo mkakati uliopo ni kuhakikisha siti zote elfu 60 katika uwanja wa Taifa zinakaliwa

Simba imejijengea rekodi ya kipekee inapocheza uwanja wa Taifa.

Msimu huu imefanikiwa kushinda michezo yake yote iliyocheza kwenye dimba hilo katika michuano ya ligi ya mabingwa

Miongoni mwa timu ambazo zilichezea kichapo ni Al Ahly, mabingwa mara nane wa taji la ligi ya mabingwa na vigogo wa soka barani Afrika

Al Ahly iliifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo wa duru ya kwanza lakini ilishindwa kufua dafu ilipokuja ‘kwa Mkapa’

Morali hiyo iliyotumika kwa Al Ahly ndio hiyo itakayotumika kuimaliza Vita Club ambayo pia ilishinda kwa mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa DR Congo

Katika mchezo huo Simba haina cha kupoteza, kwani matokeo yoyote tofauti na ushindi yataiondosha mashindanoni.

Hivyo hakuna shaka vijana wa Aussems watacheza mpira wa kushambulia mwanzo mwisho

Kocha Patrick Aussems amewaalika mashabiki wote wa soka Tanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa Jumamosi ili kuweza kuandika Historia pamoja na Simba