Aussems asaka dawa ya kupata matokeo ugenini

Droo ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika imefanyika jana nchini Misri Simba ikipangwa kukipiga na TP Mazembe katika hatua hiyo

Simba itaanzia nyumbani kwa kuikaribisha TP Mazembe kwenye dimba la Taifa mchezo utakaopigwa kati ya April 05/06 na mchezo wa marudiano kupigwa Lubumbashi DR Congo kati ya April 12/13 2019

Simba imejipambanua kwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kushinda michezo yote ya ligi ya mabingwa iliyocheza kwenye dimba la Taifa msimu huu, hivyo hakuna wasiwasi TP Mazembe hawatatoka salama uwanja wa Taifa

Hata hivyo vijana wa Patrick Aussems wamekuwa na wakati mgumu wanapokwenda ugenini. Wamefanikiwa kushinda mchezo mmoja tu dhidi ya Mbabane Swallows na kupoteza michezo mingine yote

Katika hatua ya makundi Simba iliruhusu mabao 12 ugenini huku pia ikishindwa kufunga bao lolote

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema ili waweze kutinga nusu fainali ni lazima wafanye vizuri nyumbani halafu wahakikishe hawafanyi vibaya ugenini

Amesema wamekuwa wakiyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo ya ugenini na anaamini wataweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe

Hata hivyo Aussems amesema Simba imevuka malengo iliyojiwekea kwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Amesema michuano ya msimu huu imewasaidia kubaini mapungufu yao hasa kwa michezo ya ugenini na watayafanyia kazi ili msimu ujao wawe imara zaidi