Aussems aahidi Simba tofauti Lubumbashi

Kikosi cha Simba tayari kimeondoka nchini kuelekea Lubumbashi DR Congo kwa ajili ya mchezo wa marudiano robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya TP Mazembe


Simba itashuka katika dimba la Mazembe kesho kuumana na wenyeji wao hao ambao mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa waliwalazimisha suluhu ya bila kufungana
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba kushindwa kupata ushindi katika dimba la Taifa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu
Hata hivyo licha ya matokeo hayo kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania Patrick Aussems amesema wana nafasi kubwa ya kupata matokeo yatakayowapeleka nusu fainali huko Lubumbashi

Aussems amesema mchezo waliocheza Dar umemsaidia kutambua udhaifu wa wapinzani wao na amerekebisha makosa yaliyosababisha wakose ushindi nyumbani
Amewataka mashabiki wa Simba na Watanzania wote kuwaombea huku akiahidi kuwa wataishuhudia Simba tofauti kabisa na ile ambayo ilipoteza michezo yote ya ugenini katika hatua ya makundi
Aussems amesema mbinu atakazotumia kwenye mchezo huo wa marudiano zitawashangaza Wakongo nyumbani kwao, licha ya kukiri ni pambano gumu.

Kocha huyo alisema wamegundua kwenye mchezo wa kwanza viungo wao walishindwa kumiliki mpira na washambuliaji kupoteza nafasi nyingi kizembe na kuwapa nafasi Mazembe kuwatawala, lakini wanapoenda kuwafuata kwao viungo wake na washambuliaji watakuwa na kazi maalum Lubumbashi.

“Hatutakiwi kufanya makosa ya kupoteza mpira katika sehemu ya kiungo, pia tukienda mbele tutatakiwa kuwa na malengo makubwa tutawalazimisha wafanye makosa, tuko katika utofauti mkubwa ukilinganisha na mechi za nyuma tulizocheza ugenini,” amesema

Simba imeondoka na kikosi cha wachezaji 18 ikitumia usafiri wa ndege ya kukodi. Itarejea jijini Dar es salaam kesho baada ya mchezo huo