Makambo aipania Mtibwa Sugar

Heritier Makambo ameifungia Yanga mabao 15 kwenye ligi msimu huu akihitaji kufunga bao moja zaidi ili aweze kumfikia Salum Aiyee anayeongoza mbio za ufungaji bora akiwa amefunga mabao 16

Wakati ligi ikielekea ukingoni, mbio za kuwania kiatu cha dhahabu zimeendelea kupamba moto, Makambo akihitaji kutumia vyema michezo saba iliyobaki kufunga mabao mengi

Amefunga mabao matatu katika michezo miwili iliyopita na ameahidi kuendeleza moto wa mabao huko mkoani Morogoro Yanga itakapoikabili Mtibwa Sugar keshokutwa

Mcongomani huyo anawania nafasi ya kuitwa kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo kitakachoshiriki fainali za michuano ya AFCON 2019 zitakazofanyika mwezi Juni nchini Misri

Mwezi uliopita Makambo aliitwa kwenye kikosi cha awali cha DR Congo lakini hakufanikiwa kupenya kwenye orodha ya kikosi cha wachezaji 23 kilichoifunga Liberia 1-0 na kukata tiketi ya fainali hizo ambazo Tanzania pia itashiriki baada ya kusubiri kwa miaka 39