Bodi ya ligi yatahadharishwa mechi za saa nane

Mtaalamu wa misuli ya mwili wa binadamu Dk Kitambi Mganga ameishauri Bodi ya ligi kuu kuwa makini na utaratibu wa kupanga michezo ya ligi kuu saa nane mchana wakati wa jua kali

Dk Mganga amesema kitaalam, muda huo sio mzuri kwani unaweza ukasababisha madhara makubwa kwa wachezaji yakiwemo matukio ya vifo

“Wachezaji wanapocheza wakati wa jua kali wanakuwa katika hali ya kukausha maji mwilini kwa haraka na hivyo kuwepo na hatari ya kupatwa na shambulio la moyo au kuziba moyo na misuli kukakamaa,” amesema

“Shambulio la moyo linatokana na mwili kulazimishwa kufanya kazi ngumu wakati wa jua kali, moyo unaziba, ulimi unatoka nje, misuri inashindwa kufanya kazi ni hatari kubwa mchezaji anaweza kupoteza maisha uwanjani kama hakutakuwa na mtaalamu mwenye kujua atoe huduma gani”

Dk Mganga ambaye ni Daktari wa Coastal Union, amesema kama kuna ulazima wa kuchezesha mechi hizo katika muda huo basi mwamuzi anaweza kutenga hata dakika moja ya kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji utaratibu ambao hutumika kote duniani ambapo mchezo husimamishwa kwenye dakika ya 25-30 kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji

Msimu huu baadhi ya michezo ya ligi kuu imekuwa ikipigwa saa nane mchana ili kutoa nafasi kwa michezo mingi kuonyeshwa ‘mbashara’ na Azam TV

Michezo ya ligi iliyopigwa jana ambayo ilihusisha Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga na Coastal Union dhidi ya Simba, ilipigwa saa nane mchana ili kuepusha muingiliano wa ratiba na michuano ya AFCON U17 inayoendelea jijini Dar es salaam