Tunahitaji ushindi dhidi ya Alliance Fc – Mkude

Kiungo Jonas Mkude amesema wanafahamu hawana nafasi ya kufanya makosa zaidi kwani wanahitaji kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Simba iko mkoani Mwanza ambapo leo itachuana na Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba

Akizungumza baada ya mazoezi ya jana jioni, Mkude alisema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar, wanahitaji kupata matokeo dhidi ya Alliance Fc leo

“Hakuna mechi rahisi katika Ligi Kuu, lakini timu itakayokuwa na nidhamu uwanjani ndiyo yenye asilimia kubwa ya kupata pointi tatu muhimu. Tunahitaji kuwa kwenye ubora wetu ili tuweze kushinda kesho (leo)” amesema

Aidha, Mkude alisema hakuna timu inayoingia uwanjani kwa ajili ya kufungwa, ila anayeruhusu kufanya makosa ndiyo yanaweza kuwagharimu na hatimaye kupoteza mchezo.

“Tumekuja kupambana, mechi zetu hizi zimekuwa zinatizamwa sana na wapinzani wetu, tukifanya vizuri itatusaidia kutetea ubingwa tunaoushikilia na hiyo ndiyo mipango yetu”

Baada ya mechi ya leo, Simba itaendelea kubaki jijini Mwanza kusubiri mchezo dhidi ya KMC FC utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba pia.