Ushindi dhidi ya Alliance umetuongezea morali – Niyonzima

Kiungo Haruna Niyinzima amesema ushindi wa mabao 2-0 waliopata jana dhidi ya Alliance Fc umewaongezea morali wachezaji na wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanatetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Niyonzima aliye katika kiwango bora, aliifungia Simba bao la kwanza na baadae Okwi kuongeza la pili katika kipindi cha pili

“Mchezo haukuwa rahisi hasa kutokana na matokeo tuliyopata kwenye mchezo uliopita, tulikuwa na presha ya kupata ushindi,” amesema Niyonzima

“Tunashukuru tumefanikiwa kuondoka na alama zote tatu, matokeo haya yametuongezea morali ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo”

Akizungumzia ugumu wa ratiba, Niyonzima amesema Simba ilisajili wachezaji 30 hivyo anaamini wataweza kukabiliana na changamoto ya kucheza kila baada ya siku mbili au tatu

“Kocha alituambia atakuwa akifanya mabadiliko ya kikosi ili kuhakikisha kila mchezaji anahusika. Hii ndio faida ya kusajili wachezaji wengi”

“Najua haitakuwa kazi rahisi lakini naamini tutafanikiwa kutetea ubingwa”

Simba imebaki jijini Mwanza ambapo kesho itashuka tena kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikabili KMC