TMA yatoa tahadhari ujio wa kimbunga Keneth

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa leo Alhamisi

Kwa mujibu wa TMA, jana kimbunga hicho kilikuwa kilomita 450 kutoka pwani ya Mtwara na kina kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi leo Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara.

Kwa mujibu wa TMA, eneo husika ambalo kimbunga hicho kitatua litakuwa nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara.

Hata hivyo, mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususani mikoa ya Lindi na Ruvuma yataathirika pakubwa (athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara).

TMA imetahadharisha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu na nguvu kubwa (ya upepo na mvua) itakayopelekea madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

“Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibufu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali. Uharibifu wa mazao mashambani na miundombinu kutokana na mafuriko”