Viongozi hakikisheni Yanga inamaliza msimu salama

Mpaka hapa ilipofika Yanga hata kama haitatwaa ubingwa wa ligi kuu, msimu huu utabaki kuwa wa mafanikio kwa mabingwa hao wa kihistoria

Licha ya kukabiliwa na changamoto za kiuchumi, wachezaji wa timu hiyo wamepambana na kuweza kufanya vizuri kwenye ligi huku wakitinga nusu fainali ya michuano ya kombe la Azam (ASFC)

Mwanzoni mwa msimu hakuna aliyeipa Yanga nafasi ya kufanya vizuri kutokana na kushindwa kufanya usajili ‘mkubwa’ ukilinganisha na wapinzani wake Simba na Azam Fc

Bila shaka mgomo waliofanya wachezaji juzi umewasikitisha wengi, ni faraja kusikia uongozi wa timu hiyo umechukua hatua haraka kuirejesha timu katika hali ya kawaida

Wachezaji na benchi la ufundi wamefanya kazi kubwa katika mazingira magumu, litakuwa jambo la kusikitisha kama walichokifanya wakati wa shida kitaharibiwa dakika hizi za majeruhi

Naamini viongozi wameyasikia malalamiko ya wachezaji, wayapatie ufumbuzi mapema ili wamalize msimu kwa moyo mmoja

Yanga bado inawania mataji mawili, wakati huu inapaswa fikra za wachezaji ziwe katika kumaliza msimu kwa nguvu ili washinde angalau taji moja kuliko kufikiria mambo mengine