Nyoni aahidi pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons

Beki kiraka wa Simba Erasto Nyoni amesema wamefuata alama sita mkoani Mbeya, alama tatu walizipata jana na kesho watapambana kuhakikisha wanapata alama nyingine tatu dhidi ya Tanzania Prisons

Licha ya changamoto ya ukaribu wa michezo yake, Nyoni amesema wataendelea kujituma ili kupata matokeo yatakayo-wahakikishia kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita

Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City jana, kesho Jumapili Simba itarudi tena uwanja wa Sokoine kuikabili Tanzania Prisons

Simba itahitaji kuwa katika ubora wake ili kuondoka na ushindi dhidi ya Prisons iliyoimarisha kiwango chake tangu ilipoanza kunolewa na kocha Adolph Richard

Aidha mazingira ya uwanja wa Sokoine yanaweza kuchangia kuharibu burudani kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo

Hata hivyo Nyoni amesema kama walifanikiwa kupata ushindi dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja huo, basi watahakikisha wanashinda mchezo dhidi ya Prisons

“Hali ya uwanja hatuwezi kuikwepa lakini jambo la msingi kwetu tutahakikisha tunapambana. Tunawaahidi mashabiki wetu kuwa tumedhamiria kushinda mchezo huo,” amesema