Baada ya kusambaa kwa taarifa za mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo kusajiliwa na Horoya AC ya Guinea kwa mkataba wa miaka mitatu, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla alifafanua kuwa dili hilo limeihusisha klabu yake na Makambo aliondoka nchini na Kocha Mwinyi Zahera
Hata hivyo imefahamika Zahera alilekea nchini Bennin ambako amekwenda kufanya mazungumzo na mshambuliaji mwingine
Halitakuwa jambo la kushangaza kama mshambuliaji huyo atakuwa Marcellin Koukpo ambaye alikuja msimu uliopita lakini usajili wake kukwamishwa na wajanja wachache waliokuwa wakitaka ‘ten percent’
Koukpo mshambuliaji wa Kimataifa wa Benin, alikaa nchini kwa zaidi ya wiki mbili kabla ya kuamua kuondoka baada ya kupishana na viongozi wa Yanga
Mshambuliaji huyo alipendekezwa na aliyekuwa kocha wa Yanga msimu uliopita, George Lwandamina na alifanyiwa majaribio na kocha Mwinyi Zahera kabla ya kuibuliwa taarifa za ‘uzushi’ kuwa ameshindwa majaribio
Baada ya kumuuza Makambo, Yanga inaweza kusajili washambuliaji wawili ambapo mmoja anaweza kuwa huyo Mbenin huku timu hiyo ikihusishwa na mshambuliaji wa Gor Mahia Jacques Tuyisenge na Roderick Matuma raia wa Zimbabwe anayekipiga kunako klabu ya Fc Lupopo
Dirisha la usajili litafunguliwa mwezi ujao ambapo uongozi wa Yanga umepania kukiimarisha kikosi chake wakijipanga kutumia kati ya Bil 1.5 hadi Bil 2
Hata hivyo Yanga imedhamiria kukamilisha masuala ya usajili mapema hasa ikizingatiwa Zahera ndiye msimamizi Mkuu wa mchakato huo
Mwanzoni mwa mwezi wa sita Zahera atarejea kwao Congo kwa ajili ya majukumu ya timu ya Taifa kuelekea fainali za AFCON zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 2019