Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ndanda Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa uwanja wa Taifa.
Ndanda Fc ilitangulia kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya 16 mfungaji akiwa Nasor Hasimu baada ya timu hiyo kufanya shambulizi la kushitukiza.
Yanga ilirejea mchezoni kwenye dakika 24 ilipofanikiwa kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na kiungo Jaffar Mohammed aliyeichezea yanga kwa mara ya kwanza leo kwenye ligi
Bao hilo lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib aliyerejea kwenye kikosi cha Yanga leo baada ya kukosa michezo miwili iliyopita akisumbuliwa na maumivu ya mgongo
Ndanda iliyocheza kwa kujihami zaidi, ilitumia mashambulizi ya kushitukiza ambayo mara kwa mara yalipelekea hatari langoni kwa Yanga na kumlazimu mlinda lango Beno Kakolanya kufanya kazi ya ziada
Kwenye kipindi cha pili Yanga ilitawala mchezo huo kwa muda mwingi na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni kwa Ndanda lakini kukosekana umakini kwa safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Heritier Makambo kuliikosesha Yanga mabao
Matokeo hayo yanaibakisha Yanga katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi licha ya kuwa na alama 26 sawa na Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao.
