Imeripotiwa kuwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga Obrey Chirwa anaelekea klabu ya Azam Fc baada ya kuwekewa ngumu na kocha wa Yanga Mwinyi Zahera.
Mshambuliaji huyo inaelezwa atasaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam wiki ijayo dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Chirwa alikuja nchini kwa mwaliko wa Yanga akitokea nchini Misri baada ya kuvunja mkataba wake katika klabu ya Nogoom El Mostakbal FC inayoshiriki ligi daraja la pili.
Inadaiwa Yanga imekamilisha mazungumzo na mshambuliaji kutoka nchini Ghana ambaye ni mmoja wa wachezaji wanne waliotajwa na kocha Zahera kuwa wanaweza kutua Yanga wakati wa dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Alhamisi ijayo
Kutokana na wasiwasi ulioonyeshwa na kocha Zahera juu ya tabia ya Chirwa, inaelezwa uongozi wa Yanga umeamua kuachana nae.
Azam Fc ilikuwa ikihusishwa na Chirwa hata kabla hajatimkia nchini Misri.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Hans van Pluijm ambaye ndiye aliyemleta Chirwa Tanzania wakati akiinoa Yanga, amependekeza mshambuliaji huyo asajiliwe na Azam.
Chirwa sasa atakwenda kuungana na mshambuliaji mwingine aliyetokea Yanga Donald Ngoma ambaye amepona majeraha yake na tayari ameifungia timu hiyo mabao matatu kwenye ligi