Baada ya kutua Azam Fc mshambuliaji wa zamani wa Yanga Obrey Chirwa amesema hana kinyongo na kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera aliyemuwekea ngumu kurejea Jangwani.
“Kocha alisema mimi simtaki Chirwa sababu ana tabia ya kugoma. Ni kweli mimi niko hivyo hivyo na siwezi kubadilika,” Chirwa aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kutambulishwa na Azam Fc.
“Mpira ni kazi yangu, kama silipwi stahiki zangu lazima nidai kwa njia yoyote. Na kama nikishindwa nitavunja mkataba”
“Sina tatizo na kocha wala klabu ya Yanga, ninamtakia kila la kheri aweze kuipa mafanikio Young Africans,” amesema
Katika hatua nyingine Chirwa ameeleza kushangazwa na wachezaji wengi hapa nchini kutokana na kushindwa kuwa na misimamo jambo ambalo linawafanya waendelee kuzipigania timu zao bila kulipwa chochote.
“Unajua wachezaji wengi hapa nchini wamekosa msimamo wa kulinda mikataba yao, niko tayari kuvunja mkataba wangu na kwenda mahala pengine ninapoona stahiki zangu hazilipwi kwasababu nina familia na inanitegemea” alisema.