Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kurejea kwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, Baraza la Wadhamini limeridhia kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura lakini habari zaidi zinasema Manji atahudhuria mkutano huo wa kwanza.
Kamati ya utendaji ya Yanga juzi iliagizwa na Baraza la Wadhamini kuandaa mkutano mkuu na haraka utekelezaji wake umefanyika.
Jana jioni Baraza la Wadhamini la Yanga limeridhia kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Novemba 24.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema Baraza la Wadhamini ambalo jana pia lilikutana kwa ukamilifu liliridhia mkutano huo.
Taarifa zaidi zinasema katika mkutano huo, Manji amekubali kushiriki katika mkutano huo ambao kama atafika basi utakuwa mkutano wake wa kwanza tangu atangaze kujiuzulu.
“Tumefanya mkutano na kukubaliana ni bora tufanye mkutano wa dharura ili tuweze kuwekana sawa na mikutano kama hii ndiyo muhimu kutuunganisha,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji.
“Tunataraji pia mwenyekiti wetu Manji amethibitisha kuhudhuria, wanaotaka kusikia kauli yake basi wajiandae kumsikia siku hiyo.”