Alhamisi, November 15 2018 keshokutwa ndio siku ambayo dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa.
Vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara vitakuwa na nafasi ya kuboresha vikosi vyao ili kuhakikisha vinafanya vizuri msimu huu.
Yanga ni miongoni mwa timu ambazo zinalazimika kulitumia vyema dirisha hilo ili kurekebisha mapungufu yaliyoonekana na benchi la ufundi.
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alisema timu yake inahitaki kusajili wachezaji wanne wanaocheza nafasi za beki, kiungo, winga na mshambuliaji.
Zahera ambaye yuko DR Congo kwa majukumu ya timu ya Taifa alisema tayari amewaachia viongozi wa Yanga kazi ya kukamilisha usajili wa wachezaji hao.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga Hussein Nyika alisema wamekusudia kukamilisha usajili wa wachezaji wote waliopendekezwa na kocha Zahera.
Zahera aliyefanikiwa kuiongoza Yanga kucheza zaidi ya miezi mitatu bila ya kufungwa amesema kama wachezaji hao watapatikana, timu hiyo itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kurejesha ubingwa wake uliokwenda Msimbazi msimu uliopita.
Wengi wamekuwa wakijiuliza Yanga ina pesa za kukamilisha usajili huo?
Nyika hakuwa tayari kulizungumzia hilo lakini amesisitiza anachojua yeye ni kuwa watawasajili wachezaji waliopendekezwa na Zahera.