Kuna wakati kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alifichua kuwa mshambuliaji Heritier Makambo alifukuzwa Hotelini alikokuwa amepanga kutokana na uongozi wa Yanga kushindwa kulipa kodi ya pango
Makambo alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga wenye madai ya fedha za mishahara hadi miezi minne achilia mbali malimbikizo ya bonasi na fedha za usajili
Lakini changamoto hizo hazikumuondoa katika majukumu yake, alijituma kwa moyo mmoja kuhakikisha Yanga inafanya vizuri
Dili nono alilopata klabu ya Horoya AC ni matunda ya uvumilivu na kujituma kwake katika klabu ya Yanga
Hili ni somo kwa wachezaji wengine Yanga hasa wale wenye malengo ya kufika mbali
Migomo na ‘kususa’ kucheza haviwezi kuwasaidia kufikia malengo hayo
Nakumbuka mwanzoni mwa msimu Zahera alikaa na wachezaji wote na kuwaeleza umuhimu wa wao kuifanya kazi kwa bidii bila ya kujali changamoto zinazowakabili
Bila shaka hawa akina Makambo walimuelewa vizuri na ndio maana walifanya kazi kwa bidii, leo wameona matunda yake
Wachezaji wa Kitanzania wajenge utamaduni wa kuwa na malengo ya kufika mbali
Leo hii ukimuangalia Beno Kakolanya alichokipata baada ya kuigomea Yanga utamsikitikia tu
Kama Beno angeendelea kucheza Yanga pengine leo angekuwa kipa namba moja wa kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’
Beno aliigomea Yanga wakati kiwango chake kikiwa juu sana na tayari alishaitwa kikosi cha timu ya Taifa
Angecheza michuano ya AFCON 2019 na kuwa na nafasi kubwa ya kuonekana Kimataifa na kujiongezea nafasi ya kupata timu nje ya nchi
Hawa akina Makambo wawe somo kwa wachezaji wetu.
Wawe makini katika kufanya maamuzi, wajitambue, wawe wavumilivu na kuwa na malengo ya kufika mbali
Muhimu zaidi watafute Wasimamizi ambao wanaweza kuwasaidia kufikia malengo yao