Ukiachilia mbali zawadi nyingi ambao uongozi wa klabu ya Simba utawapa wachezaji baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo, jana Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohammed Dewji ‘Mo’ aliahidi kuwapa kila mchezaji Bodaboda yenye thamani ya Tsh Mil 2.4
Mo alisema zawadi hiyo itawasaidia wachezaji na familia zao kwani ni kitega uchumi kizuri
“Zawadi hii ya Bodaboda kwa kila mchezaji naitoa mimi mwenyewe. Nimewaambia wachezaji watumie Bodaboda hizo kama kitega uchumi na kuwapa ndugu zao ili kujiingizia kipato kila siku,” amesema Mo
“Wanaweza kuingia mikataba na ndugu zao ambao hawana kazi na kujipatia Tsh 15,000/- mpaka pale mikataba hiyo inapomaliza”
“Nimefarijika na mafanikio tuliyopata msimu huu. Umoja na Mshikamano baada ya kuanza uongozi mpya ni chachu ya mafanikio haya”
“Nimethamini kilichofanywa na wachezaji wetu msimu huu ndio maana nimeamua kuwapa zawadi hiyo kila mmoja”
Bilionea huyo amesema msimu ujao wamejipanga kupata mafanikio zaidi ambapo safari hii timu inatarajiwa kwenda kuweka kambi Ureno au Marekani
Simba inatarajiwa kuingia kambini mara tu baada ya kumalizika fainali za michuano ya AFCON 2019 inayofanyika nchini Misri
Wachezaji nane wa kikosi cha Simba wanatarajiwa kushiriki michuano hiyo