Mwekezaji wa klabu ya Simba Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema hivi karibuni atatoa Bilioni 20 za uwekezaji wa klabu hiyo

Mwekezaji wa klabu ya Simba Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema hivi karibuni atatoa Bilioni 20 za uwekezaji wa klabu hiyo alizoahidi kuzitoa baada ya kushinda zabuni

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mo amesema changamoto ya urasimishaji wa mali za Simba imepelekea yeye kuchelewa kutoa fedha hizo

“Simba haikuwa na nyaraka halisi zake yakiwemo majengo na uwanja wa Bunju. Uongozi ulilazimika kufanya kazi ya ziada kupata hati halisi kwa mujibu wa sheria, ” alisema Mo

“Lakini pia Simba ilikuwa na madeni Mamlaka ya Mapato (TRA), klabu ilitakiwa kupeleka hesabu kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu. Kwa sasa zoezi hilo limekamilika na hata hati halisi za mali za klabu zimekamilika hivyo kukamilisha mchakato wa kufanikisha zoezi la uwekezaji”

Mo alisema anatarajia kuanza kutoa fedha zilizomo ndani ya mkataba wa uwekezaji muda mfupi ujao baada ya mchakato wa uwekezaji kukamilika

Tangu Simba ilipofanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake, Mo amekuwa akitoa fedha zote za kuiendesha timu hiyo ikiwemo kulipa mishahara ya wachezaji pamoja na mambo mengine yanayohusu fedha

Baada ya ligi kumalizika, Mo ameahidi kukiboresha kikosi cha Simba ambapo amesema fedha zitakazotumika kwenye usajili ni zaidi ya zile zilizotumika msimu uliopita

Msimu uliopita Simba ilitumia Tsh Bilioni 1.3 katika usajili

Leave a comment