Sina tatizo na Tshabalala – Manula

Nahodha Msaidizi wa Simba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ juzi alisababisha ‘majanga’ baada ya kujifunga bao pekee lililoihakishia Kagera Sugar ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya Simba

Tshabalala alichanganyana na mlinda lango Aishi Manula hali iliyopelekea wote watokee majaro iliyokuwa imechongwa kutoka wingi ya kushoto tukio lilisababisha Tshabalala aujaze mpira kimiani

Baada ya tukio hilo, Manula alimvaa Tshabalala na wawili hao ‘kushikana mashati’ kabla Mlipili hajaingilia kati kumuondoa Tshabalala eneo la tukio

Manula amesema tukio lililotokea uwanjani kati yao lilisababishwa na presha ya mchezo lakini liliishia palepale uwanjani, hawana tatizo nje ya uwanja

“Hatukuwa na mawasiliano mazuri,” amesema Manula ambaye pia ni mlinda lango namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania

“Kilichotokea pale kilisababishwa na presha ya mchezo tu, Tshabalala ni rafiki yangu na tumekuwa tukishirikiana katika masuala mbalimbali”

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alilizungumzia tukio hilo ambapo alisema limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uchovu wa wachezaji wake ambao wamekuwa wakicheza mfululizo

“Tumecheza michezo saba ndani ya siku 16, wachezaji wangu ni binadamu, wanachoka. Ndio maana baadhi ya matukio wanayofanya yanasameheka kwa kuwa najua yanasababishwa na mazingira yanayotukabili”

Wawa arejea kikosini Simba

Beki kisiki wa Simba Paschal Serge Wawa amerejea kikosini baada ya kuwa nje kwa mwezi mmoja akiuguza majeraha ya nyama za paja

Wawa tayari ameanza kujifua na kikosi cha Simba kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Azam Fc utakaopigwa kesho

Hata hivyo Wawa hatarajiwi kushuka dimbani kesho kwa kuwa amepewa program maalum ya mazoezi ya pekee yake ambao ametakiwa kuyafanya kwa siku nne

“Nimeanza mazoezi. Kwa sasa nafanya mazoezi ya peke yangu kwa siku nne kabla ya kujiunga na wenzangu,” amesema

Wawa aliumia kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe uliopigwa April 06 katika uwanja wa Taifa

Beki huyo mkongwe huenda akarejea kikosini kwenye mchezo dhidi ya Ndanda Fc na bila shaka atakuwepo Simba itakapochuana na Sevilla kwenye mchezo wa kirafiki, May 23

Mzee Muchacho na Fahad wambananisha Haji Manara avae jezi ya Yanga SC

Afisa Habari wa Simba SC Haji Manara kuelekea mchezo wa nusu fainali ya UEFA Champions League aliahidi kuwa endapo Liverpool itaitoa FC Barcelona katika hatua hiyo basi atahama timu kutoka Simba SC na kwenda Yanga, sasa leo akakutana na mashabiki wa Liverpool Mzee Muchacho na Fahad wanamtaka atimize ahadi yake.
Ndio wanabishana na kusema kuwa Fahad atimize kwana ahadi yake ya kutobolewa macho aliyowahi kuitoa ndio Haji Manara nae atavaa jezi ya Yanga, Fahad na Mzee Muchacho wakawa wanamlazimisha Haji Manara aombe radhi kwa kushindwa kutimiza ahadi hiyo.

Aiyee awanyooshea mikono Kagere, Okwi na Bocco

Straika wa Mwadui FC,Salim Aiyee amewataja nyota wa Simba, Meddie Kagere, Emanuel Okwi na John Bocco mmoja wapo kubeba tuzo ya mfungaji bora, huku akimchomoa Heritier Makambo wa Yanga kwenye vita hiyo msimu huu.

Aiyee ambaye alianza kwa kasi msimu huu na kuongoza kwa muda mrefu kwenye orodha ya ufungaji mabao kwa kupachika 16, kwa sasa ameshaachwa nyuma mabao manne na Straika wa Simba Meddie Kagere.

Kagere amefunga mabao 20, Makambo ana mabao 16 sawa na Aiyee (Mwadui) na Bocco akiwa na 14 sawa na Okwi wote wa Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Straika huyo alisema kwa hali ilivyo ni wazi nyota wa Simba, Kagere, Okwi na Bocco mmojawapo anaweza kubeba tuzo hiyo lakini kwa Makambo wa Yanga hawezi kufurukuta.

Alisema sababu ya kuwapa nafasi wachezaji wa Simba ni kutokana na kuwa na mechi nyingi lakini hata kombinesheni yao inatisha sana lakini pia wana uwezo hata kiuchumi.

“Sijakata tamaa, lakini kiukweli Kagere, Okwi na Bocco mmoja wapo anaweza kubeba tuzo ya mfungaji bora, Makambo hapana hayumo kabisa, wale Simba kombinesheni yao ni nzuriîalisema Aiyee.

Pia mshambuliaji huyo alieleza kuwa kupungua kwa kasi yake kwenye ufungaji mabao ni kutokana na mechi nyingi za ugenini kuwa na changamoto nyingi ikiwamo kukamiwa, alikiri ushindani msimu huu umekuwa mkali kutokana na ongezeko la timu.

Aussems ataka Niyonzima aongezewe mkataba

Kocha mkuu wa Simba Patrick Aussems amependekeza klabu hiyo kumuongezea mkataba wa miaka miwili kiungo wake fundi Haruna Niyonzima ambaye anatarajia kumaliza mkataba wake mwezi ujao

Aussems amesema anamuhitaji Niyonzima kwa ajili ya msimu ujao

Amesema Niyonzima ameimarisha kiwango chake na angependa kuendelea kuwa nae kwenye kikosi chake kwa muda mrefu

Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio ya kikosi cha Simba katika michuano ya ligi ya mabingwa ambayo Simba ilitolewa hatua ya robo fainali

Aussems ahakikishiwa mkataba mpya Simba

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems atasaini mkataba mwingine wa kuendelea kuifundisha timu hiyo baada ya mkataba wake wa awali kumalizika imefahamika

Aussems aliyetua Simba mwezi Julai mwaka jana, ametimiza masharti aliyopangiwa msimu uliopita ambapo alitakiwa kuifikisha timu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa pamoja na kutwaa taji la ligi kuu

Chini yake Simba imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa na iko mbioni kukamilisha sharti la pili la kutwaa ubingwa wa ligi kuu

Inaelezwa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake Mohammed Dewji ‘Mo’ itampa Aussems mkataba wa mwaka mmoja na atasaini mkataba huo kabla ya kurejea kwao kwa ajili ya mapumziko baada ya ligi kumalizika

Ubingwa bado unaenda Simba, mechi tatu kuamua

Licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar jana, hesabu za kutwaa ubingwa kabla ya kucheza na Sevilla ziko palepale

Keshokutwa Jumatatu May 13 Simba itashuka uwanja wa Uhuru kucheza na Azam Fc katika mchezo ambao mabingwa hao watetezi wanahitaji ushindi

Katika mchezo wa duru ya kwanza Azam Fc ilipokea kichapo cha mabao 3-1

Baada ya mchezo huo Simba itacheza na Mtibwa Sugar May 16 kisha kucheza na Ndanda Fc May 19 michezo yote ikitarajiwa kupigwa uwanja wa Uhuru

Ushindi katika michezo hiyo mitatu utaifanya Simba ifikishe alama 90 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine

Aidha lengo la kukabidhiwa kombe kwenye mchezo dhidi ya Sevilla litafanikiwa kama Simba itashinda michezo hiyo iliyobaki

Simba imeshuka dimbani mara 32, inaongoza ligi ikiwa imejikusanyia alama 81 ikifuatiwa na Yanga yenye alama 80

Uchovu umechangia kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wemepoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar leo kutokana na changamoto mbalimbli likiwemo suala la uchovu kwa wachezaji wake

Aussems amesema wamecheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi hivyo baadhi ya makosa yaliyofanywa na wachezaji wake yanasameheka

Nahodha Msaidizi Mohammed Hussein alijifunga bao pekee lililoipa Kagera Sugar ushindi wa bao 1-0

“Nawapongeza Kagera Sugar kwa kupata ushindi leo. Tulifanya makosa tukajifunga, tumepata nafasi kadhaa za kufunga tukashindwa kuzitumia, tumekubali matokeo ndio mpira,” amesema

“Kikosi changu kinakabiliwa na uchovu pamoja na majeruhi ya baadhi ya wachezaji. Tunajitahidi kuwapa mapumziko wachezaji lakini sasa tunakabiliwa na changamoto nyingine ya mfungo wa Ramadhani, wachezaji wengine wamefunga”

“Kabla ya mchezo wa leo tumeshinda michezo 18 kati ya 19 tuliyocheza, kufungwa ni jambo la kawaida, nampongeza kocha wa Kagera Sugar kwa kushinda leo”

Licha ya kupoteza mchezo wa leo, Simba inahitaji kushinda michezo mitatu kati ya sita iliyobaki ili kutetea ubingwa