Uchovu umechangia kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wemepoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar leo kutokana na changamoto mbalimbli likiwemo suala la uchovu kwa wachezaji wake

Aussems amesema wamecheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi hivyo baadhi ya makosa yaliyofanywa na wachezaji wake yanasameheka

Nahodha Msaidizi Mohammed Hussein alijifunga bao pekee lililoipa Kagera Sugar ushindi wa bao 1-0

“Nawapongeza Kagera Sugar kwa kupata ushindi leo. Tulifanya makosa tukajifunga, tumepata nafasi kadhaa za kufunga tukashindwa kuzitumia, tumekubali matokeo ndio mpira,” amesema

“Kikosi changu kinakabiliwa na uchovu pamoja na majeruhi ya baadhi ya wachezaji. Tunajitahidi kuwapa mapumziko wachezaji lakini sasa tunakabiliwa na changamoto nyingine ya mfungo wa Ramadhani, wachezaji wengine wamefunga”

“Kabla ya mchezo wa leo tumeshinda michezo 18 kati ya 19 tuliyocheza, kufungwa ni jambo la kawaida, nampongeza kocha wa Kagera Sugar kwa kushinda leo”

Licha ya kupoteza mchezo wa leo, Simba inahitaji kushinda michezo mitatu kati ya sita iliyobaki ili kutetea ubingwa

SIMBA YAENDELEZA UTEJA MBELE YA KAGERA SUGAR YAKUBALI KICHAPO CHA BAO 1-0

Kagera Sugar imeendeleza umwamba dhidi ya Simba baada ya leo tena kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru


Bao la kujifunga la beki Mohammed Hussein katika dakika ya 42 liliihakikishia Kagera Sugar alama tatu muhimu ambazo huenda zikawanusuru na janga la kuteremka daraja

Licha ya kosakosa kadhaa kutoka kwa Simba, mchezo huo ulimalizika kwa vijana wa Meckie Mexime kupata ushindi wa pili dhidi ya Simba msimu huu

Hata hivyo bado Simba iko kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya Yanga nayo kuchezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Biashara United

Mchezo unaofuata ni dhidi ya Azam Fc, utapigwa May 13 katika uwanja wa Uhuru

Simba yaita mashabiki uwanja wa Uhuru

Uongozi wa klabu ya Simba umewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanja wa Uhuru leo wakati mabingwa hao wa nchi watakapokuwa wakichuana na Kagera Sugar

Simba inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuendelea kuukaribia ubingwa ambapo wanahitaji kushinda michezo minne tu

Msemaji wa Simba Haji Manara amesema baada ya kupoteza mchezo wa mkoani Kagera, leo ni zamu ya Wana Msimbazi kufurahi kwenye dimba lao la nyumbani

“Kutesa kwa zamu, zamu yao iliishia Kagera na sisi leo zamu yetu. Wanasimba tujitokeze kwa wingi kuwashangilia wachezaji wetu mwanzo wa mchezo hadi mwisho,” amesema

Licha ya hali ya hewa ya mvua inayoendelea kunyesha jijini Dar es salaam, mchezo huo utapigwa kama ulivyopanga

Simba kuendelea na msako wa ubingwa uwanja wa Uhuru leo

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo wanashuka uwanja wa Uhuru kuikabili Kagera Sugar ukiwa ni mchezo wa ligi raundi ya 35

Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, utakuwa wa kisasi kwa Patrick Aussems na vijana wake baada ya kupoteza mchezo wa duru ya kwanza

Leo Simba imepania kumaliza ‘uteja’ kwa Kagera Sugar inayonolewa na kocha Meckie Mexime

Mexime ameshinda michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba

Msimu uliopita Kagera Sugar iliharibu sherehe ya Simba kukabidhiwa ubingwa baada ya kushinda kwa bao 1-0 mbele ya Rais Magufuli na viongozi waandamizi wa Serikali na klabu ya Simba

Lakini pia msimu huu Kagera Sugar ilishinda mchezo uliopigwa uwanja wa Kaitaba

Kikosi cha timu hiyo kiko jijini Dar es salaam tangu Jumatatu kikijiwinda na mtanange huo wa kukata na shoka

Matokeo ya ushindi kwa Simba yatazidi kuwasogeza karibu ya ubingwa wa pili mfululizo kwani wanahitaji kushinda michezo minne tu kati ya saba iliyobaki

Hesabu za Aussems ni kwenye ubingwa tu

Baada ya ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union, kikosi cha Simba kinaendelea na maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Kagera Sugar

Mchezo huo utapigwa kesho Ijumaa, May 10 kwenye uwanja wa Uhuru

Kocha Mkuu wa vinara hao wa ligi kuu Patrick Aussems amesema lengo la kwanza la kuongoza ligi tayari limefanikiwa na sasa wanahitaji kukamilisha lengo la pili la kutetea ubingwa

“Lengo kubwa ni kutetea ubingwa na sasa tunaongoza ligi tukiwa na michezo mitatu nyuma ya wapinzani wetu,” amesema Aussems

“Mimi naangalia zaidi timu yangu na mpinzani wangu ajae ni Kagera Sugar, timu nyingine sijali”

Simba inahitaji kushinda michezo minne tu ili kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Michezo yote minne inayofuata itapigwa uwanja wa Uhuru.

Baada ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar michezo inayofuata ni dhidi ya Azam Fc, Ndanda na Mtibwa Sugar

Hatma ya Okwi kujulikana mwishoni mwa msimu

Mshambuliaji hatari wa Simba Emmanuel Okwi amesema hatma yake ya kuendelea kukipiga Msimbazi itafahamika mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapokuwa umemalizika kabisa

Okwi amekuwa akihusishwa kutakiwa na klabu za Orlando Pirates na Kaizer Chiefs zinazoshiriki ligi kuu ya Afrika Kusini

Mwishoni mwa mwaka jana klabu ya Kaizer Chiefs ilituma ofa kwa Simba kutaka kumsajili mshambuliaji huyo, ofa ambayo ilikataliwa na uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania

Jana baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union Okwi aligoma kuweka hadharani hatma yake akibainisha kuwa mazungumzo yatafanyika mwishoni mwa msimu na lolote linaweza kutokea

Uongozi wa Simba tayari umeanza mazungumzo na wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu

Mbali na Okwi, wachezaji wengine ambao mikataba yao iko ukingoni ni pamoja na Aishi Manula, John Bocco, Erasto Nyoni, Nicolas Gyan, Shomari Kapombe na Jonas Mkude

Okwi ataja siri ya kurejesha makali yake ya ufungaji

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Simba Emmanuel Okwi jana alifunga mabao matatu sawa na Meddie Kagere na kuisaidia Simba kupata ushindi mnono wa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union

Hiyo ilikuwa hat-trik ya pili kwa Okwi msimu huu

Kwa siku za karibuni Okwi amekuwa katika kiwango bora cha kuzifumania nyavu, kwa wastani akifunga karibu kila mchezo

Okwi aliuanza msimu kwa kasi akifanikiwa kufunga mabao saba katika michezo ya mwanzoni mwa msimu

Hata hivyo baadae alijikuta akishindwa kuzifumania nyavu kwa karibu miezi mitatu hali iliyopelekea wakosoaji wake kupata la kuzungumza

Lakini tangu Simba iondoshwe hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Okwi amezaliwa upya na amekuwa akitupia mabao nyavuni kila anapojisikia

Okwi amefichua kilichomsaidia ni uvumilivu na ushirikiano anaoendelea kupata kutoka kwa wachezaji wenzake

“Wakati nilipokuwa sifungi sikukata tamaa, nilijua ni kipindi cha muda tu ambacho kitapita” amesema Okwi

“Wenzangu waliendelea kunipa moyo na kunihamasisha nijitume zaidi”

“Lakini jambo jema ni kuwa Simba haitegemei mchezaji mmoja. Kila anayepata nafasi anaweza kufunga ndio maana mimi nsipofunga wapo wengine watafunga, tunacheza kwa kushirikiana”

Kagere, Bocco, Okwi, mabao 48 miguuni mwao

Wakati walipokuwa wakisajiliwa na Simba wapo walioponda usajili wao kuwa umri umewatupa mkono na hawataweza kuwa na msaada kwa Simba

Lakini mpaka sasa wao watatu, nahodha John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wamefunga mabao 48 kati ya 69 yaliyofungwa na Simba msimu huu

Kagere ndiye anayeshikilia usukani wa mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa amefunga mabao 20 wakati Bocco na Okwi wote wamefunga mabao 14

Msimu huu Simba tayari imeshaweka rekodi tatu muhimu; moja ni timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye mchezo mmoja (8-1) na pili ni timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwa ujumla mpaka sasa (69) na tatu ni timu iliyoruhusu mabao machache (13)

Kama itashinda michezo yote saba ilyobaki, Simba itaweka rekodi ya kufikisha alama 102. Mpaka sasa inahitaji kushinda michezo minne tu ili kuweza kutetea ubingwa