Kikosi cha Yanga vs Ruvu Shooting

1. Ramadhani Kabwili
2. Paulo Godfrey
3. Haji Mwinyi
4. Andrew Vicent
5. Abdallah Shaibu
6. Feisal Salum
7. Ibrahim Ajib
8. Papi Tshishimbi
9. Heritier Makambo
10. Amissi Tambwe
11. Jaffar Mohammed

SUB
Klaus Kindoki
Juma Abdul
Gadiel Michael
Cleofas Sospeter
Maka Edward
Pius Buswita
Deus Kaseke

Tshishimbi, Yondani kuongeza Nguvu kikosini Yanga

Nahodha wa Yanga Kelvin Yondani amerejea kikosini baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki tatu akisumbuliwa na majeraha ya enka.

Hivi karibuni Yondani na mlinda lango Beno Kakolanya waliviteka vyombo vya habari za michezo baada ya kudaiwa wamegoma kucheza wakishinikiza walipwe madai yao.

Hata hivyo beki huyo mkongwe alikanusha taarifa hizo na kusisitiza alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya enka na uongozi wa Yanga ulikuwa na taarifa zake

Naye kiungo Mcongomani Papi Tshishimbi amerejea kikosini baada ya kupona majeraha.

Tshishimbi, Yondani na winga mpya Reuben Bomba walihudhuria mazoezi ya jana ya kikosi cha Yanga yanayofanyika Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es salaam.

Simba Yapewa tahadhari juu ya NKANA FC

Simba imetinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kibabe kwa kuifumua Mbabane Swallows jumla ya mabao 8-1 katika michezo miwili ya hatua ya awali.

Ushindi huo umeongeza mzuka na kujiamini kwa kikosi cha Simba ambacho kimedhamiria kutinga hatua ya makundi.

Simba itachuana na Nkana Fc ya Zambia katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ambapo itaanzia ugenini mjini Kitwe wiki ijayo Disemba 14 2018.

Kuelekea mchezo huo wadau na wachambuzi mbalimbali wa soka nchini wameitahadharisha Simba kuwa ni lazima ijipange sawasawa kuweza kuiondosha Nkana Fc kwani timu hiyo sio ya kubezwa.

Pia historia baina ya timu hizo inafanya mchezo baina yao kuwa na ushindani wa aina yake. Nkana ilianzishwa mwaka 1935 wakati Simba ilianzishwa mwaka 1936

Timu zote zinatumia jezi za rangi nyeupe na nyekundu.

Mwaka 1990 Nkana Fc ilitinga fainali za michuano ya ligi ya mabingwa wakati Simba ilitinga fainali za michuano ya kombe la Washindi mwaka 1993

“Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Simba na Nkana kukutana kwenye michuano mikubwa barani Afrika,” amesema Ally Mayay mmoja wa wachambuzi wa soka katika runinga ya Azam

“Simba na Nkana zilishawahi kukutana miaka iliyopita. Ifahamike kuwa Nkana ilishafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1990, lakini pia ina wachezaji wengi kutoka nchi zilizoendelea kisoka tofauti na Simba,” amesema

“Ili Simba waweze kushinda mbele ya Nkana, ni lazima wajipange upya kwa kurekebisha makosa ambayo yalijitokeza hususan kwenye safu ya ulinzi ambayo licha ya kutofungwa kwenye mechi za kwanza, lakini inahitaji maboresho kwani wangekutana na timu nzuri wasingefika walipo sasa”

Naye Kenny Mwaisabula amesema Simba inapaswa itambue kila wanaposonga mbele katika michuano hiyo ndio ugumu unaongezeka hivyo wanapaswa kujipanga.

“Simba bado ina kazi kubwa na kila wanavyosonga mbele lazima wajue ndio ugumu wa mashindano unavyoongezeka, hivyo benchi la ufundi linatakiwa kukaa na wachezaji ili kuwaeleza nini kilichopo mbele yao”

“Ni vema Simba wakaenda kucheza mechi hiyo kwa tahadhari kubwa kwani Nkana ni timu nzuri kuliko hata Mbabane, wana uzoefu wa mashindano na wamekuwa wakifanya vema katika mechi nyingi za kimataifa”

Simba itakuwa inasaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Nkana ambayo wamewahi kukutana nayo mara mbili huko nyuma.

Hata hivyo awamu hii Simba imeonekana kuwa na kikosi imara ambacho kinao uwezo wa kuwaondosha Wazambia hao na kutinga hatua ya makundi

PICHA: Simba sc ilivyowasili Tanzania

Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba kimewasili leo Alhamisi mchana kutoka eSwatini kutimiza majukumu ya Kimataifa.

Mashabiki wengi wamejitokeza kuwalaki wekundu hao wa Msimbazi ambao wamefanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.