SIMBA : Yaapa kuikomalia JS Saoura LEO

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba wako nchini Algeria ambapo leo Jumamosi March 09 2019 watashuka dimba la Agosti 20 kuikabili JS Saoura katika mchezo wa ligi ya mabingwa utakaopigwa saa nne usiku

Simba inaweza kuandika historia nyingine leo kwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu

Mashabiki wa Simba na Watanzania wote kwa ujumla wametakiwa kuiombea timu dua njema ili iweze kupeperusha vyema bendera ya nchi huko ugenini

Aidha mafanikio ya Simba kwenye michuano hii ni mafanikio ya Tanzania kwani iwapo itafanikiwa kusonga mbele, itaiongezea Tanzania alama na pengine msimu ujao nchi inaweza kuongezewa idadi ya wawakilishi kwenye michuano hiyo

Kwa sasa Tanzania ina nafasi mbili tu kwenye michuano ya CAF wakati baadhi ya nchi zina nafasi hadi nne kutokana na vilabu vyao kufanya vizuri

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema vijana wake wana ari ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo

“Hatukuja hapa kwa malengo ya kutafuta sare, tunataka kushinda mchezo huu,” amesema Aussems

Ushindi unaweza kuihakikishia Simba kutinga robo fainali kama Vital Club itashindwa kupata ushindi dhidi ya Al Ahly katika mchezo utakaopigwa mapema saa moja jioni

Lakini hata alama moja itaifaa Simba kuelekea mchezo wake wa mwisho dhidi ya Vita Club utakaopigwa uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo March 16 2019

SIMBA SC: Yatua Algeria Kuivaa JS SAOURA

Msafara wa wachezaji, benchi la ufundi, baadhi ya viongozi wa klabu ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati ya Mashindano, Ahmed Mgoyi umewasili salama mjini Algiers, Algeria na kupokelewa na Balozi wa Tanzania wa Algeria, Omary Mzee. #NguvuMoja

KAGERE: Aibuka Mchezaji BORA | Mwezi Februari | TUZO

Mshambuliaji wa timu ya Simba, Meddie Kagere amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

Kagere raia wa Rwanda ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Salim Aiyee wa Mwadui na Salum Kimenya wa Prisons alioingia nao fainali.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohamed Rishard kuwa Kocha Bora wa mwezi Februari akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Mwadui, Ally Bizimungu.

Juuko ana kadi tatu za njano, Okwi mgonjwa, Nyoni hayuko ‘fit’

Katika orodha ya wachezaji 20 ambao jana walisafiri kuelekea nchini Algeria kwa ajili ya mchezo dhidi ya JS Saoura yamekosekana majina ya wachezaji watatu muhimu ambao ni Juuko Murshidi, Erasto Nyoni na Emmanuel Okwi

Wakati Okwi aliondolewa kikosini kutokana na kuwa hajapona vizuri majeraha yake, Juuko anatumikia adhabu ya kadi za njano

Baada ya mchezo dhidi ya Stand United, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems alitaja sababu ya kutomtumia beki Erasto Nyoni ambaye ameanza mazoezi hivi karibuni akitoka kwenye majeraha ya goti

Aussems alisema Nyoni bado ‘hayuko fit’ na atahitaji muda zaidi ili kuweza kurejea kwenye kiwango chake.

Kutokana na umuhimu wa mchezo dhidi ya JS Saoura, Aussems amelazimika kusafiri na wachezaji ambao wana utimamu wa mwili kwa asilimia 100