Okwi, Nyoni wanogesha mazoezi Simba

Kiraka Erasto Nyoni na mshambuliaji Emmanuel Okwi leo walikuwepo uwanjani wakijifua na kikosi cha Simba kinachojiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita takaopigwa Jumamosi, March 16 katika uwanja wa Taifa

Simba iliyorejea jana kutoka Algeria inajifua kwenye uwanja wa Boko Veterans

Nyoni na Okwi hawakusafiri na Simba ilipokwenda nchini Algeria kumenyana na JS Saoura kutokana na kuwa majeruhi

Wachezaji hao leo wamejumuika na wachezaji wengine wakihusika katika program zote za mazoezi hivyo kuongeza matumaini kuwa wako tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi

SIMBA SC Yatua DAR

Makamanda wetu wamewasili nchini salama. Jumamosi watakuwa Uwanja wa Taifa kutoa burudani kwa Wanasimba na Watanzania wote. Hii ni #DoOrDie #NguvuMoja ✊🏽

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama, tuna mchezo mwingine tutacheza na AS Vita, mimi naamini kabisa kwa morali tuliyonayo na mbinu za kocha tukiwepo nyumbani tutapambana na tutafuzu”- Nahodha John Bocco baada ya kuwasili nyumbani 🇹🇿. #DoOrDie #NguvuMoja ✊🏽

MO DEWJI: Tukutane Taifa

Mwekezaji wa klabu ya Simba Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ amewataka mashabiki wa timu hiyo na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo wataki Simba itakapochuana na Vita Club

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Mo amesema kwa sasa hapendi kuzungumza maneno mengi lakini anawaita uwanja wa Taifa mashabiki wa Simba Watanzania wote kuiunga mkono Simba katika mchezo huo muhimu

“Sina maneno mengi, tukutane uwanjani wanaSimba na waTanzania wote kwa ujumla,” ameandika Mo

Katika michezo yote msimu huu ambayo Mo yuko uwanjani, Simba imeibuka na ushindi.

Licha ya kuwa mwekezaji, Mo amejipambanua kuwa shabiki na muhamasishaji namba moja wa klabu ya Simba kuelekea ‘gemu’ kubwa

SIMBA vs AS VITA

Viingilio vya mchezo wa mwisho wa hatua makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita Club ambao tutacheza siku ya Jumamosi Machi 16, 2019. #YesWeCan #NguvuMoja

Maeneo ambayo tiketi za mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita Club zinauzwa.

SIMBA SC : DUBAI – DAR

Msafara wa wachezaji, benchi la ufundi, baadhi ya viongozi wa klabu ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati ya Mashindano, Ahmed Mgoyi umefika salama Dubai. Leo usiku watalala kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Dubai na asubuhi wataendelea na safari ya kurejea nyumbani Tanzania. #NguvuMoja

Alikufa Al Ahly uwanja Taifa, Vita ni nani

Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya JS Saoura Jumamosi iliyopita kwa kufungwa mabao 2-0, Jumamosi ijayo Simba inarejea kwenye uwanja wa Taifa kumaliza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwa kuikabili AS Vita Club

Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote kwenye mchezo huo ili iweze kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili katika historia yake

Simba iliwahi kutinga robo fainali ya michuano hiyo mwaka 1974

Kwenye msimamo wa kundi D JS Saoura inaongoza ikiwa imejikusanyia alama nane ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama saba sawa na Vita Club ambayo inashika nafasi ya tatu

Simba inashika nafasi ya nne ikiwa na alama sita

Bila ya kujali matokeo kati ya Al Ahly dhidi ya JS Saoura, ushindi utaihakikishia Simba kufikisha alama tisa na kujihakikishia moja ya tiketi mbili za kutinga robo fainali

Habari njema kwa Simba ni kwamba itakuwa ikicheza mchezo huo mbele ya mashabiki wake ambapo mkakati uliopo ni kuhakikisha siti zote elfu 60 katika uwanja wa Taifa zinakaliwa

Simba imejijengea rekodi ya kipekee inapocheza uwanja wa Taifa.

Msimu huu imefanikiwa kushinda michezo yake yote iliyocheza kwenye dimba hilo katika michuano ya ligi ya mabingwa

Miongoni mwa timu ambazo zilichezea kichapo ni Al Ahly, mabingwa mara nane wa taji la ligi ya mabingwa na vigogo wa soka barani Afrika

Al Ahly iliifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo wa duru ya kwanza lakini ilishindwa kufua dafu ilipokuja ‘kwa Mkapa’

Morali hiyo iliyotumika kwa Al Ahly ndio hiyo itakayotumika kuimaliza Vita Club ambayo pia ilishinda kwa mabao 5-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa DR Congo

Katika mchezo huo Simba haina cha kupoteza, kwani matokeo yoyote tofauti na ushindi yataiondosha mashindanoni.

Hivyo hakuna shaka vijana wa Aussems watacheza mpira wa kushambulia mwanzo mwisho

Kocha Patrick Aussems amewaalika mashabiki wote wa soka Tanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa Jumamosi ili kuweza kuandika Historia pamoja na Simba

HAJI MANARA

Kuelekea mechi yetu ya jumamosi dhidi ya AS Vita leo saa sita na nusu mchana ntaongea na Wanahabari Kwenye makao makuu ya klabu yaliyopo msimbazi

Do or Die

FT : JS Saoura 2-0 Simba

Simba imepoteza mchezo wake wa tatu ugenini baada ya kufungwa mabao 2-0 na JS Saoura katika mchezo wa ligi ya mabingwa raundi ya tano uliopigwa nchini Algeria

Wenyeji waliutawala mchezo huo, ushindi ni matokeo yanayoakisi walichokifanya katika dimba lao la nyumbani

Licha ya kufungwa vijana wa Patrick Aussems walionekana kuimarika ukilinganisha na michezo mingine miwili ya ugenini ambayo waliruhusu mabao 10

Matokeo hayo yameishusha Simba mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa kundi D wakibaki na alama zao sita

JS Saoura wamechupa mpaka nafasi ya kwanza baada ya kufikisha alama nane

Al Ahly inashika nafasi ya pili ikiwa na alama saba sawa na Vita Club inayoshika nafasi ya tatu Al Ahly ikifaidika na matokeo baina ya timu hizo

Mapema leo Vita Club iliilaza Al Ahly bao 1-0 wakati Al Ahly ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Misri

Simba sasa ni lazima ishinde mchezo wa mwisho dhidi ya Vita Club, mchezo ambao utapigwa Jumamosi ijayo kwenye uwanja wa Taifa

Kimahesabu bado Simba ina nafasi ya kutinga robo fainali