Simba kuifuata Coastal Union Jumatatu

Msafara wa kikosi cha Simba unatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kesho Jumatatu kuelekea mkoani Tanga kuikabili Coastal Union kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Mchezo huo wa kwanza baina ya timu hizo msimu huu, utapigwa siku ya Jumatano, April 17 kwenye uwanja wa Mkwakwani

Baada ya kumaliza majukumu ya michuano ya CAF, Simba imedhamiria kutetea ubingwa wake kuhakikisha inapata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao

Simba imerejea nchini usiku wa kuamkia leo ikitokea DR Congo ambako iliondoshwa na TP Mazembe kwenye michuano ya ligi ya mabingwa hatua ya robo fainali

Serengeti Boyz yapoteza mchezo wa kwanza AFCON U17

Timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boyz, imeanza vibaya michuano ya AFCON U17 inyofanyika nchini baada ya kukubali kipigo cha mabao 5-4 kutoka kwa Nigeria katika mchezo uliopigwa uwanja wa Taifa

Licha ya kupoteza mchezo huo, Serengeti Boyz ilicheza vizuri na hakika hawapaswi kulaumiwa

Edmund John aliifungia Serengeti Boyz mabao mawili moja likiwa la mkwaju wa penati huku mengine mawili yakifungwa na Kelvin John ‘Mbappe’ na Morice Abraham (p)

Vijana wa Nigeria walifunga mabao yao kupitia kwa Olatomi, Ubani aliyefunga mabao mawili, Amoo na Abraheem

Mchezo unaofuata wa Serengeti Boyz ni April 17 dhidi ya Angola kabla ya kumaliza hatua ya makundi kwa kuchuana na Uganda April 20

TETESI: Usajili SIMBA SC

Klabu ya Simba Sc inatarajia kuanza kulifanyia kazi pendekezo la kocha wake Mkuu Patrick Aussems kuwania saini ya beki wa kushoto wa Yanga Sc Gadiel Michael ili kurithi mikoba ya Asante Kwasi ambaye anaonekana kuwa dhaifu kwasasa mbele ya Mohamed Hussein. .
.
Inasemekana klabu hiyo itaachana na Asante Kwasi na kwa mujibu wa kocha mkuu wa klabu hiyo amependekeza jina la Gadiel Michael kuchukua nafasi hiyo
.
.
Mkataba wa Gadiel na Yanga Sc unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Wanachama Yanga wakumbushwa kuhakiki majina yao

Yanga iko ndani ya mchakato wa uchaguzi ambao utahitimishwa May 05 mwaka huu kwa Wanachama wa klabu hiyo kuchagua viongozi wapya

Uongozi wa Yanga umewataka viongozi wa Matawi kuwakumbusha wanachama wahakiki majina yao kwenye ‘ledger’ zilizo kwenye matawi yao

Wanachama wa Yanga pia wamekumbushwa kulipia ada za uanachama ili kuwa na sifa ya kuchagua viongozi katika uchaguzi utakaofanyika May 05

Uchaguzi utahusisha wanachama wote wenye kadi za kitabu na wale wenye kadi za posta.

Ten awapiga ‘dongo’ Simba, ‘vumilieni ndio ukubwa huo’

Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amewataka mashabiki wa Simba wavumilie ‘madongo’ wanayovurumishiwa baada ya jana kufumuliwa mabao 4-1 na TP Mazembe na kuondoshwa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika hatua ya robo fainali

Kutupwa nje ya michuano hiyo kwa Simba kuliibua shangwe kubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga na hii inatokana na Simba kutumia mafanikio yao msimu huu ‘kuwanyanyasa’ watani zao Yanga ambao wanapita katika kipindi kigumu

Ten amesema Yanga na Simba ni watani wa jadi hivyo ni vyema wakavumilia matani wanayokutana nayo mtaani kwani na wao wamekuwa wakifanya hivyo wakati wote ambao Yanga inakumbwa na changamoto

“Ndiyo Sisi na ninyi ni watani na tunataniana kweli hasa timu zetu zinapokosa matokeo,” ameandika Ten kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram

“Bahati mbaya ni kwamba ninyi mnapenda kutania wenzenu lakini mkitaniwa ninyi ‘Nongwa’ mnahamia kwenye kashfa..! Mkikashifiwa nanyi mnaanza kulialia”

“Hongereni kwa hatua mliyofika, muhimu ni kuangalia wapi mmekosea ili mfanikiwe zaidi siku za usoni”

“Wakati sisi tunajiuliza nanyi mjiulize zaidi. Msimvuruge @moodewji ili aendelee kuwabeba..!”

Aidha Ten amewakaribisha Simba kwenye ligi kuu huku akiwatupia ‘dongo’ kuwa mitandao yao ya simu itakuwa imejaa tayari kwa kufanya miamala

“La huko limeisha, mrudi bongo sasa najua simu zenu zina line mbili mbili yaani full network kama siyo Mpesa basi Tigopesa…!”

Baada ya kutolewa Simba inarejea kwenye ligi ikikumbana na rundo la ‘viporo’ ambavyo watatakiwa wavimalize ndani ya kipindi cha mwezi mmoja

Katika kipindi hicho Simba wanapaswa kucheza michezo 16 kwani ligi imepangwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa tano ili kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ambayo mwezi Juni inaelekea Misri kushiriki fainali za AFCON 2019

Njooni mtuunge mkono mchezo dhidi ya Nigeria – Nahodha Serengeti Boyz

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boyz leo kinashuka dimba la Taifa kuikabili Nigeria kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya AFCON U17, mchezo utakaopigwa saa kumi kamili jioni

Tanzania ni mwenyeji wa michuano hiyo inayoanza kutimua vumbi leo katika viwanja vya Azam Complex na Taifa

Nahodha wa kikosi cha Serengeti Boyz Morris Michael amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa watakapokuwa wakiikabili Nigeria leo

“Nimezungumza na wenzangu na kuwashusha presha kwamba tunaenda kucheza mchezo wa kawaida kama michezo mingine ambayo tumecheza, kwa hiyo tuuone wa kawaida,” amesema

“Ni mechi kubwa lakini hatutakiwi kuwa na presha, tunatakiwa kupambana hadi mwisho kupata ushindi.”

“Tukishinda mchezo huu tutapata picha nzuri ya matarajio yetu hapo mbele tofauti na tukipoteza au kupata sare.”

“Watanzania waje kutuunga mkono kwa sababu tupo nyumbani naamini tutafanya kitu ambacho watanzania hawataamini”

Viingilio vya mchezo huo VIP ni Tsh 5,000/- na upande wa mzunguuko ni Tsh 2,000/-