NIYONZIMA: Tutacheza fainali ya ligi ya mabingwa

Kiungo Haruna Niyonzima amesema Jumamosi ya March 16 2019 ilikuwa siku ya kipekee kwake na klabu ya Simba baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Niyonzima anayetajwa kuwa nyota wa mchezo wa siku hiyo ambao Simba iliilaza AS Vita Club mabao 2-1, amefichua kuwa licha ya kupata majeraha punde tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi katika dakika ya 58, amesema alilazimika kuvumilia na kuhakikisha anaitumia vyema nafasi aliyopewa na kocha Patrick Aussems

“Nilijipa moyo na kusema siwezi kuruhusu majeraha haya yakanifanya nitoke nje. Nimekuwa nikijituma ili nipate nafasi kama hii,” amesema Niyonzima

“Tangu nikiwa mdogo nimekuwa na ndoto ya kucheza fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Hakuna kitakachonizuia kutimiza ndoto hiyo na pia sikuwa tayari kuwaangusha mashabiki wa Simba na Watanzania pamoja na ndugu zangu Wanyarwanda”

“Tuna nafasi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa mwaka huu, bila shaka tutaweza kwani tuna kikosi cha kufanikisha hilo pamoja na mashabiki wanaotuunga mkono muda wote”

Aussems alia na mazoezi ya Stars

Kocha Mkuu wa timu ya Simba Patrick Aussems ameingiwa na hofu kutokana mazoezi wanayopewa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kuwa yanaweza kupelekea majeruhi

Aussems ametoa tahadhari hiyo hasa ikizingatiwa kwenye kikosi cha Stars Simba ina wachezaji wanne

Wachezaji wa Simba walioitwa kikosi cha Stars ni Aishi Manula, Jonas Mkude, John Bocco na Erasto Nyon

Ikumbukwe mwishoni mwa mwaka jana Simba ilimpoteza beki wake Shomari Kapombe ambaye yuko nje kwa zaidi ya miezi mitano akiuguza majeraha aliyopata akiwa katika kambi ya Stars Afrika Kusini

Simba inakabiliwa na michezo ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, droo ya hatua hiyo ikiatarajiwa kufanyika nchini Misri kesho

Kocha Mkuu wa Stars Emannel Amunike ameanza kukinoa kikosi cha Stars jana, wachezaji wakifanya mazoezi mara mbili kwa siku

Stars inajiandaa kuikabili Uganda Jumapili, March 24 2019

Simba kuivaa Ruvu Shooting bila nyota kibao

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba leo jioni watashuka katika dimba la Taifa kuikabili Ruvu Shooting kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Katika mchezo huo utakaopigwa saa moja jioni, Simba itawakosa baadhi ya nyota wake ambao wameitwa kujiunga na timu za Taifa

Nahodha John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Aishi Manula wameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda Cranes utakaopigwa mwishoni mwa wiki

Meddie Kagere ameitwa kikosi cha Rwanda wakati Emannuel Okwi na Juuko Murshid wao wameitwa kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema atafanya mabadiliko madogo ya kikosi chake kitakachoshuka dimbani leo

Amewatoa wasiwasi Wanamsimbazi kuwa watafanya vizuri katika mchezo huo lengo likiwa ni kuondoka na alama zote tatu

SIMBA vs RUVU SHOOTING

Baada ya juzi kuitoa Tanzania kimasomaso kwa kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, kikosi cha Simba kesho Jumanne kitakuwa dimba la Taifa kuikabili Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa saa moja jioni

Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 51

Hata hivyo ina michezo tisa ya viporo hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wake kama itashinda yote

Simba kuiongeza Tanzania nafasi michuano ya CAF

Mafanikio ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa, yameinyanyua Tanzania hadi nafasi ya 12, ambayo ndiyo ya mwisho katika orodha ya nchi zinazopewa nafasi 4 katika mashindano ya Afrika.

Kabla ya msimu huu, Tanzania ilikuwa nafasi ya 26 na pointi zake 3 zilizotokana na Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, 2016 na 2018.

Kufuzu kwa Simba robo fainali msimu huu, kumeipatia nchi yetu pointi 15 ambazo zikichanganywa na zile 3 za Yanga, tunakuwa na pointi 18

POINTI

CAF hupima viwango vya nchi kupitia mafanikio ya vilabu vyake, kwenye mashindano ya Afrika, kwa kipindi cha miaka mitano.

Viwango vipya vitakavyotoka vikijumuisha mafanikio ya Simba 2018/19, vitaanzia 2015.

Mwaka wa karibuni zaidi huwa na thamani kubwa zaidi (maksi 5) kuliko mwaka wa nyuma zaidi (maksi 1).

Thamani ya mwaka wa mashindano huzidishwa na pointi ambazo klabu huzipata kutokana na mafanikio yake kwenye mashindano husika, na kuwa pointi za nchi.

KOMBE LA SHIRIKISHO

Klabu itakayoshika nafasi ya 4 kwenye makundi, hupewa pointi 0.5. Nafasi ya 3, pointi 1, robo fainali, pointi 2, bingwa pointi 5.

Yanga ilifuzu hatua ya makundi mwaka 2016 na 2018, na kumaliza ya 4 mara zote mbili.

Thamani ya mwaka 2016 ni maksi 2, maana yake ni 0.5 × 2 = 1. Thamani ya mwaka 2018 ni maksi 4, maana yake ni 0.5 × 4 = 2.

Kwa hiyo Tanzania ilivuna pointi 3 kutokana na mafanikio ya Yanga, 2016 na 2018!

LIGI YA MABINGWA

Kufuzu makundi tu ni pointi 0.5 na kufika robo fainali ni pointi 3. Simba imefika robo fainali 2018/19 ambao thamani yake ni maksi 5. Maana yake ni 3X5=15.

Pointi hizi 15 zikijumlishwa na zile 3 za Yanga, Tanzania inakuwa na pointi 18.

Hata hivyo, pointi hizi zitaingia kwenye mahesabu kuanzia msimu ujao kwa ajili ya matumizi ya msimu wa mbele yake, yaani 2020/2021.

Hakuna uwezekano wa pointi zetu kuvukwa na nchi nyingine kwa sababu walio chini yetu hawana timu zilizopo kwenye mashindano.

Pia ukiangalia hapo kwenye mchoro, utaona pointi zetu zimewekewa alama ya ≥…hii ina maana kwamba zinaweza kuongezeka, endapo Simba watasonga mbele zaidi.

2020/21 tutaingiza timu nne michuano ya vilabu barani Afrika!

CC : Zakazakazi