SEVILLA : Kutua Na Msafara wa watu 60

Timu ya Sevilla kutoka Hispania inatarajiwa kuwasili leo ikiwa na msafara wa watu 60 unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo

Sevilla ambayo itacheza na Simba mchezo wa kirafiki keshokutwa, ikiwa nchini itashiriki katika shughuli za kijamii

Safari ya Sevilla nchini imedhaminiwa na kampuni a SportPesa ambao pia ni wadhamini wakuu wa timu za Simba na Yanga

Mabingwa hao wa kihistoria wa taji la Europa, wanakuwa timu ya kwanza kutoka ligi kuu ya Hispania kutembelea Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla

Sevilla iliyotwaa taji la Europa mara tano, itacheza na Simba keshokutwa Alhamisi, May 23 katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa, saa moja jioni

TETESI ZA USAJILI SIMBA LEO JUMANNE

Tetesi za usajili Simba leo 21 May 2019

Kikosi cha Simba leo huenda kikatangaza ubingwa kikicheza kwenye ardhi ya Singida katika uwanja wa Namfua, Simba inahitaji walau sare tu ili kuweza kutangaza Ubingwa mbele ya Singida United wanaohitaji ushindi ili kujihakikishia kuendelea kusalia ligi kuu.

Ukiachana na hayo ya Simba kushinda inaelezwa kuwa kikosi cha Simba kinaendelea kutafuta wachezaji wakuimarisha kikosi chao kwaajili ya msimu ujao.

Kama ulijisahaulisha, mchezaji Vitalis Mayanga wa Ndanda inaelezwa kuwa ni suala la muda tu kutua Simba kwani Simba na Ndanda walishamalizana muda tu na kijana anasubiri ligi iishe waweze kumjumuisha kikosini.

Vitalis Mayanga licha ya kuwa akitajwa kuwaniwa na baadhi ya vilabu nchini Tanzania Yanga ikitajwa lakini imebainika ni mchezaji halali wa Simba anayesubiria ligi iishe aungane na mabingwa hao wa soka nchini.
Credit: Kwataunit

(TFF) imetangaza Waamuzi watakaochezesha mchezo wa Kirafiki wa Kimataifa Simba dhidi ya Sevilla

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza Waamuzi watakaochezesha mchezo wa Kirafiki wa Kimataifa Simba dhidi ya Sevilla ya Hispania itakayochezwa Uwanja wa Taifa Mei 23,2019.

Muamuzi wa Katikati atakua Elly Sasii,Muamuzi msaidizi namba moja Mohammed Mkono kutoka Tanga,Muamuzi msaidizi namba mbili Soud Lila wa Dar es Salaam na Muamuzi wa akiba atakuwa Jonesia Rukyaa kutoka Kagera.

Sevilla inatarajiwa kuwasili nchini kesho Jumanne tayari kwa mchezo huo wakati kikosi cha Simba kitarejea jijini Dar es salaam keshokutwa kutoka Singida baada ya mchezo dhidi ya Singida United kesho

MABAO YA MEDDIE KAGERE

Wakati akisajiliwa na Simba mwaka jana, wapo waliobeza usajili wa Meddie Kagere wakidai Simba haitanufaika na usajili wake kwa kuwa umri tayari umemtupa mkono

Hata hvyo mpaka sasa msimu unapoelekea ukingoni, hakuna hata mmoja atajitokeza kumbeza Kagere kutokana na alichokifanya katika klabu ya Simba ndani ya mwaka mmoja

Kagere ndiye kinara wa mabao kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara, jana akiitungua Ndanda Fc mabao mawili yaliyomfanya afikishe mabao 22

Kwa michezo iliyobaki, ni dhahiri Kagere ataibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwani mabao yake 22 yanamfanya aongoze kwa tofauti ya mabao sita dhidi ya wanaomfuatia, Salim Aiyee na Heritier Makambo ambaye tayari ameondoka Yanga

Kagere ameichezea Simba michezo 50 katika mashindano yote

Amefunga mabao 33 na kutoa pasi nne za mabao

Ana wastani wa kufunga zaidi ya bao moja kila mchezo

Kagere alitoa mchango mkubwa kwa kikosi cha Simba kwenye michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu, akifunga mabao sita

Kwa kushirikiana na washambuliaji wengine, John Bocco na Emmanuel Okwi, wameifanya Simba iwe moto wa kuotea mbali katika kuzifumania nyavu kwenye ligi

Watatu hao pekee wamefunga mabao 52 kati ya mabao 74 yaliyofungwa na Simba

SIMBA 2-0 NDANDA FC

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wanahesabu siku za kukabidhiwa ubingwa wa pili mfululizo baada ya leo kuichapa Ndanda Fc mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru

Wakicheza kandanda la pasi fupifupi lililojaa ufundi wa hapa na pale, Simba ilijipatia mabao yake yote mawili kwenye kipindi cha kwanza yote yakiwekwa kambani na Meddie Kagere ‘MK14’

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama 88 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 83

Yanga imebaki na michezo miwili, inahitaji kushinda yote ili kuweza kuipiku Simba lakini wakati huohuo Simba bado ina michezo mitatu mkononi

Ni muujiza pekee ambao utaifanya Simba isiweze kutwaa ubingwa!

Aidha Simba inaweza kwenda kumaliza ‘shughuli’ mkoani Singida keshokutwa itakapoivaa Singida United

Kwenye mchezo huo Simba inahitaji alama moja tu kuweza kurejea na ubingwa jijini Dar es salaam

Kinara wa mabao Meddei Kagere amezidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha dhahabu baada ya leo kufikisha mabao 22

Kagere anaongoza kwa tofauti ya mabao sita dhidi ya Heritier Makambo na SalimAiyee ambao wote wana mabao 16

AISHI MANULA Aipania SEVILLA

Mlinda lango wa Simba Aishi Manula amesema mchezo dhidi ya Sevilla una maana kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo kwani watakuwa na nafasi ya kuonyeshwa ukubwa wa timu yao

“Simba kucheza na Sevilla ndani ya uwanja wa Taifa ni jambo kubwa sana,” amesema

“Kwetu sisi wachezaji ni nafasi kubwa sana kuonyesha ubora wetu na kutimiza malengo ya timu yetu ambayo ni kufanya vizuri Kimataifa”

“Nawaalika mashabiki waje kwa wingi uwanja wa Taifa May 23 kuipa sapoti SImba, kuipa sapoti Tanzania”

Simba na Sevilla zitachuana Alhamisi, May 23 katika mchezo wa ‘kukata na shoka’ utakaopigwa uwanja wa Taifa kuanzia saa moja kamili jioni

SIMBA Kusaka Ushindi Leo Dhidi ya Ndanda FC

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka uwanja wa Uhuru kuikabili Ndanda Fc katika mchezo ambao matokeo ya ushindi yataisogeza Simba karibu ya ubingwa wa pili mfululizo

Simba inayoongoza ligi ikiwa na alama 85, inahitaji alama nne tu kutetea ubingwa kwa msimu wa pili

Kuhakikisha alama tatu zinapatikana leo, kikosi cha Simba kiliingia kambini juzi baada ya kufanya kikao na Mwekezaji wa klabu hiyo Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’

Hesabu za kocha Patrick Aussems ni kuhakikisha wanashinda mchezo wa leo na ule utakaofuata dhidi ya Singida United ili kujihakikishia ubingwa kabla ya mechi mbili za mwisho

Baada ya mchezo leo, Simba itaondoka jijini Dar es salaam kuelekea Singida ambako keshokutwa Jumanne, May 21 itacheza na Singida United

May 22 Simba itafunga safari kurejea jijini Dar es salaam ambapo May 23 inakabiliwa na mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sevilla

Sevilla inatarajiwa kuwasili keshokutwa tayari kwa mchezo huo ambao utalipaisha jina la Simba na Tanzania Kimataifa kwani utarushwa ‘mbashara’ na vituo vikubwa vya runinga duniani

Kuelekea mchezo wa leo, Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wa timu hiyo wako tayari, wanafahamu Wanamsimbazi wanahitaji ushindi