Kampeni ya changia Yanga yazinduliwa kwa kishindo, mamilioni yakusanywa

Hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuichangia Yanga iliyosimamiwa na Kamati Maalum iliyoundwa chini ya Mh Anthony Mavunde, ilifanyanyika kwa mafanikio makubwa Hotel ya Morena jijini Dodoma

Hafla hiyo iliyorushwa ‘mbashara’ na Azam Sport 2, iliwajumuisha wadau wa Yanga ambapo kupitia hafla hiyo fedha, ahadi na uhamasishaji mkubwa ulifanyika ili kuhakikisha Yanga inafikia lengo la kukusanya fedha za kutosha kwa ajili ya kukiboresha kikosi cha timu hiyo

Akifungua hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mh Mavunde alisema Kamati imeandaa mfumo mzuri wa kuwezesha upatikanaji wa fedha zitakazofanikisha mipango ya timu hiyo

“Lengo la kamati hii ni kuandaa mfumo mzuri utakaowezesha kupatikana pesa itakayofanikisha mipango ya timu yetu ikiwemo mwalimu kusajili wachezaji wazuri kwa msimu ujao,” alisema

Mavunde aliwataja miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ambao anaamini kutokana na ushawishi wao katika jamii, wataweza kuharakakisha kukamilika kwa mpango huo

“Kamati yetu ina wajumbe takribani 28, na wengine ni watu wenye ushawishi katika maeneo mbalimbali.

“Lutawatangaza hapa kila mjumbe na mkoa atakaoratibu”

“Yupo Masoud Kipanya, Jokate Mwegelo, Said Ntimizi, Maulid Kitenge, Papaa Ndama na kipenzi cha wana Yanga Abdallah Bin Kleb na wengineo.

“Tumejipanga vema, wapenzi wa Yanga mna wajibu mkubwa wa kuinga mkono kamati hii ili kufikia malengo yaliyoanishwa”

Miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo ni Mh Mwigulu Nchamba Rais wa klabu ya Singida United ambaye ni mdau mkubwa wa klabu ya Yanga

Nchemba ameahidi kusajili mchezaji mwingine kama alivyofanya kwa Feisal Salum na amemtaka kocha Mwinyi Zahera ampe jina la mchezaji mmoja miongoni mwa wachezaji nane wa kigeni ambao amepanga kuwasajili

“Kwa mara ya kwanza nimekaa na kuongea na Mwalimu wetu, hakika ana maono ya mbali na timu yetu,” alisema

“Naahidi kuendelea kuichangia klabu yangu na naomba mwalimu anipe jina la mchezaji mmoja ntamsajili kama nilivyomsajili Fei Toto”

Wengine waliotoa ahadi kubwa ni pamoja na Mh Hussein Bashe ambaye ameahidi kutumia vyombo vyake vya habari kuitangaza bure kampeni ya kuichangia Yanga

Mh Bashe pia alichangia Fedha Taslim kiasi cha Tsh Milioni 10

Mdau mwingine wa Yanga Cyprian Musiba alichangia Mil moja huku pia akiahidi kuitangaza bure kampeni ya kuichangia katika vyombo vyake vya habari

Yanga huenda ikakusanya zaidi ya Mil 500 baada ya hafla ya jana kutokana na fedha taslim na ahadi zilizotolewa

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ni miongoni mwa wageni walioalikwa kwenye hafla hiyo

Tutasaka ushindi Congo – Aussems

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema, bado wana nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali licha ya kupata suluhu na TP Mazembe nyumbani kwa sababu inawezekana.

Kauli hiyo pia imeungwa mmkono na Kocha wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe baada ya kutamka, hawawezi kushangilia mpaka watakaposhinda mechi hiyo ya marudiano itakayochezwa Aprili 13, Lubumbashi, DR Congo.

Aussems amezungumza hayo baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliochezwa leo Jumamosi Uwanja wa Taifa jIjinj Dar e Salaam.

“Nakubaliana na matokeo na kiwango walichoonyesha wachezaji wangu”

“TP Mazembe ni timu kubwa ingawa tulitakiwa kupata matokeo mazuri zaidi,” alisema Aussems.

Amesema, walipata nafasi lakini walishindwa kufunga. “Nafasi zilikuwepo lakini ndiyo hivyo, sasa tunajiandaa na mechi ya marudiano tutafanikiwa tu,”alisema Aussems.

“Kupata sare nyumbani si kitu kizuri lazima utapata mshtuko kwa sababu tulitegemea kushinda.” Kwa upande wa Kocha wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe amesema, haukuwa mchezo rahisi na mashabiki wameshuhudia mchezo mzuri, sisi tulikosa bao na simba pia walikosa.

“Tunarudi Lubumbashi kwa maandalizi mengine na tunakwenda kujipanga na kuweka nguvu tushinde,” alisema Mihayo. Kuhusu suluhu Mihayo amesema : ” Hatuwezi kushangilia sasa kwa sababu ya matokeo ya suluhu tutafurahi baada ya mchezo wa mwisho watakapopata matokeo mazuri.

” Huo ni mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Simba na TP Mazembe, mechi ya marudiano itachezwa Lubumbashi, DR Congo.

Mwanaspoti

Uzinduzi Changia Yanga kufanyika Dodoma leo

Kamati maalumu ya uzinduzi na uhamasishaji inayoongozwa na Mwenyekiti Mh Anthony Mavunde, leo itazindua rasmi kampeni ya kuichangia Yanga katika hafla itakayofanyika Hoteli ya Morena jijini Dodoma

Hafla hiyo itahudhuriwa na wabunge, wafanyabiashara, wasanii na watu maarufu ambao ni wadau wakubwa wa klabu Yanga

Itaanza saa 12 jioni

FT : Simba 0-0 TP Mazembe

Mchezo wa kwanza wa robo fainali ligi ya mabingwa kati ya Simba dhidi ya TP Mazembe umemalizika kwa suluhu ya bila kufungana

Mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, ulishuhudiwa na malfu ya mashabiki walioongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangala

Simba itajilaumu yenyewe kwa kushindwa kuibuka na ushindi licha ya kutengeneza nafasi nyingi hasa kwenye kipindi cha pili

Haikuwa siku nzuri kwa nahodha John Bocco ambaye alikosa mkwaju wa penati pamoja na nafasi nyingine mbili

Simba italazimika kupata matokeo ugenini ili kuweza kufuzu nusu fainali