Ibenge aivulia kofia Simba

Kocha Mkuu wa AS Vita Club Florent Ibenge amesema Simba ilistahili kushinda mchezo wa jana kutokana na kuwa katika kiwango bora kuliko timu yake

Vita Club ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba na kuondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika ikiiacha Simba ikitinga robo fainali

Akizungumza baada ya mchezo jana, Ibenge alisema Simba ina wachezaji wazuri

Aidha, Ibenge alifichua kuwa walimuwekea ulinzi mkali Meddie Kagere kwa kuwa ndio mchezaji waliokuwa wakimuhofia zaidi

“Simba walionyesha ushindani mkali kwetu, walicheza vizuri matokeo waliyopata walistahili, tunawapongeza,” amesema

“Kagere ndio mchezaji tuliyekuwa tunamuhofia zaidi na niliwaagiza wachezaji wangu wamchunge lakini mwisho wa siku mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa tumeadhibiwa”

Mabao ya Simba yalifungwa na Mohammed Hussein na Clatous Chama aliyefunga bao la ushindi katika dakika za lala salama

Baada ya Simba Kufuzu, Manara Atatimiza Ahadi ya Kutoisema Yanga Vibaya?

Simba imeweka historia nyingine kwa Tanzania baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika jana katika Uwanja wa Taifa.

Kwenye mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya AS Vita, Simba ilihitaji ushindi wowote ili ifuzu hatua ya robo fainali, jambo ambalo lilifanikiwa kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na Mohamed Hussein katika dakika ya 36 na Clatous Chama katika dakika ya 90 huku bao pekee la AS Vita likifungwa na Kasendu Kazidi katika dakika ya 13.

Kabla ya mchezo huo, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara aliahidi kupitia kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio kuwa endapo klabu yake itaibuka na ushindi, hatowasema mahasimu wake Yanga kama alivyokuwa akifanya hapo awali, bali atakaa kimya.

“Mashabiki wa Yanga wananihofia sana mimi, wanaogopa kuisapoti Simba kisa eti mimi nitasemaje. Sasa naahidi Simba ikishinda sitowasema Yanga, nitaishia kusema tu ‘Alhamdulillah'”, alisema Manara, Ijumaa, Machi 15.

Lakini kinachoonekana hivi sasa baada ya ushindi huo ni muendelezo wa maneno yake ya utani kwa mahasimu wake ambao amesema walikuwa wakiidharau timu yake.

Ahadi nyingine ambayo aliihidi Manara ni kuwa endapo Simba itavuka hatua hii ya makundi na kwenda robo fainali, basi yatakapomalizika mashindano hayo mwezi June, yeye ataitwa Msemaji wa Mabingwa wa Afrika.

Simba imevunja rekodi yake yenyewe kuwa klabu ya kwanza Tanzania tangu mwaka 1974 kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano

OKWI : Atoa neno kuelekea Mechi SIMBA vs AS VITA

Mshambuliaji hatari wa Simba Emmanuel Okwi amewaita mashabiki uwanja wa Taifa kuiunga mkono Simba itakapokuwa ikichuana na Vita Club katika mchezo utakaopigwa saa moja jioni baadae leo Jumamosi

“Tunawaomba mashabiki wetu mje kwa wingi uwanjani ili kutuunga mkono.

“Siku zote tumekuwa pamoja na sapoti yenu imekuwa msaada mkubwa kwetu katika michezo iliyopita,” amesema Okwi

“Tunataka tufanye hii siku pamoja. Tunaomba mje tupambane pamoja ili tukifuzu iwe tumefuzu wote pamoja”

“Njooni uwanjani tuandike historia wote. Tumejiandaa vya kutosha na tuko tayari kuipeleka Simba hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa”