Sababu ya Ajib kuachwa Dar yatajwa

Kikosi cha Yanga kiko mkoani Mara ambapo kesho kitashuka katika uwanja wa Karume kuikabili Biashara United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Hata hivyo Yanga ilisafiri bila ya nahodha wake Ibrahim Ajib ambaye aliondolewa kwenye kikosi baada ya kuugua ghafla

Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh amesema Ajib alipata maradhi wakati wakiwa kambini usiku wa kuamkia jana ambapo alipatiwa huduma ya kwanza na Dk Edward Bavu kabla ya kukimbizwa Hospitalini

Hafidh amesema hali ya kiungo huyo kinara wa kutoa pasi za mabao ligi kuu ya Tanzania Bara, inaendelea vizuri

Yanga iliwasili Musoma jana na kupokelewa kwa shangwe na mamia ya mashabiki wa timu hiyo

Makocha Yanga, Stand United na Mbeya City wapelekwa Kamati ya Nidhamu TFF

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewasilisha malalamiko mbalimbali ya kinidhamu dhidi ya viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Walalamikiwa ni kutoka katika klabu za Ligi Kuu ya Tanzania (TPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Makocha waliolalamikiwa ni Athuman Bilal wa Stand United, Mwinyi Zahera (Yanga), Nassoro Mrisho (Geita Gold FC), na Ramadhani Nsanzurwimo (Mbeya City).

Viongozi ni Herry Chibakasa wa Friends Rangers FC, Mohamed Hussein (Kagera Sugar FC),Walter Harrison (KMC) na Hussein Salehe wa Geita Gold FC wakati mchezaji aliyelalamikiwa ni Deus Tulusubya wa Pamba SC.

Kamati ya Nidhamu ya TFF itakutana Mei 12,2019

Fei Toto atakiwa Uingereza

Hivi karibuni kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike alimwagia sifa kiungo wa Yanga Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa anaweza kucheza soka barani Ulaya akiitaja FC Barcelona kuwa ni timu ambayo anaweza kucheza kabisa

Inaelezwa klabu ya Yanga imepokea maombi kutoka klabu moja ya Uingereza ambayo inamuhitaji Fei Toto akafanye majaribio

Timu hiyo ambayo haikuwekwa hadharani, imedhamiria kumsajili Fei Toto kama atafuzu majaribio hayo

Fei Toto aliyetua Yanga mwaka jana, amekuwa katika kiwango bora, akijihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Mwinyi Zahera

Inaelezwa Yanga imejipanga kusajili kiungo mwingine ikitokea Fei Toto atafanikiwa kutimkia Uingereza

Kagere, Bocco, Okwi, mabao 48 miguuni mwao

Wakati walipokuwa wakisajiliwa na Simba wapo walioponda usajili wao kuwa umri umewatupa mkono na hawataweza kuwa na msaada kwa Simba

Lakini mpaka sasa wao watatu, nahodha John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wamefunga mabao 48 kati ya 69 yaliyofungwa na Simba msimu huu

Kagere ndiye anayeshikilia usukani wa mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa amefunga mabao 20 wakati Bocco na Okwi wote wamefunga mabao 14

Msimu huu Simba tayari imeshaweka rekodi tatu muhimu; moja ni timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye mchezo mmoja (8-1) na pili ni timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwa ujumla mpaka sasa (69) na tatu ni timu iliyoruhusu mabao machache (13)

Kama itashinda michezo yote saba ilyobaki, Simba itaweka rekodi ya kufikisha alama 102. Mpaka sasa inahitaji kushinda michezo minne tu ili kuweza kutetea ubingwa

Okwi, Kagere waweka rekodi ya ‘hat-trik’ ligi kuu

Washambuliaji Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wameweka rekodi ya kufunga hat-trik mbili kwenye mchezo mmoja wa ligi kuu

Washambuliaji hao hatari wa Simba wamefunga mabao matatu kila mmoja katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 8-1

Mwamuzi wa mchezo huo Jonesia Rikiyaa aliwakabidhi mpira kila mmoja baada ya mchezo kumalizika

Hizo zilikuwa hat-trik za sita kufungwa kwenye ligi msimu huu

Kagere amefikisha mabao 20 na kujiimarisha kileleni katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwaacha Heritier Makambo na Salim Aiyee wakibaki na mabao 16

Okwi mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, amerejea katika mbio za kuwania kiatu hicho baada ya leo kufikisha mabao 14 akimfikisha mshambuliaji mwingine wa Simba John Bocco

Kagere, Okwi na Bocco wameifungia Simba mabao 48 kwa pamoja

FT : Simba 8-1 Coastal Union

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wamerejea kileleni mwa msimamo wa ligi kibabe baada ya kuifumua Coastal Union mabao 8-1 kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru

Leo ilikuwa siku ya sherehe ya mabao kwa washambuliaji wawili wa Simba Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao wamefunga ‘hat-trik’ kila mmoja

Alianza Okwi kupiga hat-trik kabla ya Kagere kupata ya kwake kwenye kipindi cha pili

Mabao mengine mawili yalifungwa na viungo Hassani Dilunga na Clatous Chama aliyefunga bao lake kwenye dakika za majeruhi

Kagere amejichimbia kileleni katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa amefikisha mabao 201 wakati Okwi amemfikia John Bocco baada ya kufikisha mabao 14

Simba ni kama imezianza sherehe za ubingwa leo na itahitaji kushinda michezo minne tu ili kutawazwa mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo

Tumetolewa FA, tutaendelea kupambana kwenye ligi – Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema baada ya kupoteza mchezo wa nusu fainali kombe la FA kwa kufungwa mabao 2-0 na Lipuli Fc leo, wanahamishia nguvu zao kwenye ligi kuhakikisha wanashinda michezo minne iliyobaki

Zahera amesema licha ya kutofanikiwa kutinga fainali, msimu huu wamevuka malengo na matarajio ya awali

“Hakuna kitu kitabadilika juu ya mipango yetu, tunahitaji kushinda mechi nne zilizobakia ligi kuu,” amesema Zahera

“Ukiangalia mpaka hapa tumefanikiwa kuliko matarajio. Mwaka huu tulianza ligi tukiomba mungu atusaidie japo tumalize nafasi ya sita au ya saba”

“Tulipaswa kumaliza nafasi ya sita au saba kutokana na changamoto tulizopitia msimu huu. Tulikubaliana tufanye nguvu tusimalize chini ya nafasi ya kumi”

“Mkiangalia tunaongoza ligi tokea mwanzo wa msimu mpaka leo. Malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi na hata kombe la FA yalikuja baada ya kuona tumeweza kufanya vizuri licha ya changamoto zilizokuwa zinatukabili”

“Kazi waliyofanya wachezaji wangu ni nzuri sana. Tutaendelea kupambana kwenye ligi ili tuweze kushinda michezo yote minne iliyobaki”

Aidha akizungumzia mabadiliko aliyofanya kwenye kipindi cha pili amesema ilikuwa ni kazima kuwatoa Ajib na Mohammed Issa na kuwaingiza Tambwe na Juma Abdul ili kwendana na aina ya uchezaji wa Lipuli Fc

“Lipuli walikuwa wengi katikati hivyo nililazimika kumuingiza Tambwe na Abdul ili kutumia mipira ya krosi kupitia pembeni kujaribu kusaka mabao ya kusawazisha”

“Mfumo huo ulitusaidia kwani tulipata karibu nafasi tatu za kuweza kufunga lakini tulikosa bahati”