Aussems afichua usajili atakaofanya

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema atakiongezea nguvu kikosi chake mwishoni mwa msimu kwa kusajili wachezaji wanne

Simba inayoelekea kutetea taji lake la ligi kuu kwa msimu wa pili mfululizo, inatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam leo wakitokea mkoani Mbeya ambako wameshinda michezo yote miwili dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons

Akizungumza baada ya mchezo jana, Aussems amesema ushindi wa bao 1-0 waliopata dhidi ya Tanzania Prisons umewaweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutetea ubingwa na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao

Amesema atakiboresha kikosi chake ili wafike mbali zaidi ya mafanikio waliyopata kwenye michuano hiyo msimu huu

Aussems ametaja maeneo ambayo atayaboresha kwa kusajili wachezaji wapya ni eneo la ulinzi (mabeki wawili), kiungo mmoja na mshambuliaji mmoja

Aidha, Aussems amesema timu yake inakabiliwa na changamoto ya kufanya vizuri Kimataifa kutokana na ukweli kuwa haipati ushindani mkubwa kutoka timu za ndani

Kagera Sugar yawahi Dar, Simba kurejea leo kutoka Mbeya

Kagera Sugar ndio timu pekee iliyopata ushindi dhidi ya Simba katika michezo minne ya kanda ya ziwa waliyocheza mabingwa hao watetezi kwenye duru ya pili

Kagera Sugar inayonolewa na kocha Mecky Mexime tayari kimewasili jijini Dar es salaam kusubiri mchezo dhidi ya Simba utakaopigwa Ijumaa, May 10

Simba wao watarejea jijini Dar es salaam leo wakitokea mkoani Mbeya ambako walifanikiwa kuchukua alama zote sita dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons

Hata hivyo kabla ya kucheza na Kagera Sugar Ijumaa, siku ya Jumatano Simba itachuana na Coastal Union katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa/Uhuru

Simba inahitaji kushinda michezo mitano tu kuweza kutetea ubingwa wake bila ya kujali matokeo ya Yanga ambayo imebakiwa na michezo minne ambayo kama wakishinda yote watafikisha alama 92

Ushindi katika michezo mitano utaifanya Simba ifikishe alama 93

TFF yapongeza uongozi mpya Yanga

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia amewapongeza Viongozi wapya wa Klabu ya Young Africans kwa kuchaguliwa kuiongoza klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne (4)

Karia amesema TFF itashirikiana na Viongozi hao katika maendeleo ya Mpira wa Miguu nchini

Wanachama wa Yanga jana walikamilisha salama mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo kwa kuwachagua Dk Mbette Mshindo Msolla kuwa Mwenyekiti na Fredrick Mwakalebela kuwa Makamu Mwenyekiti pamoja na kuchaguliwa kwa wajumbe wengine nane wa Kamati ya Utendaji

Mchezo wa Lipuli vs Yanga kuanza saa tisa na nusu

TAARIFA

Mchezo wa Nusu fainali ya ASFC uwanja wa Samora Utachezwa leo Kati ya Lipuli na Yanga utaanza saa 9:30 Alasiri (sio saa kumi) kama ilivyopangwa awali.

Hii ni kutokana na kwamba kama kutakuwa na suluhu (sare) baada ya dk 90 kutakuwa na Extra Time na baadaye penalty.

Na viingilio vya mchezo wa leo ni kama ifuatavyo

V.I.P – 20,000
MZUNGUKO 5,000
WATOTO – 2,500

Upatapo taarifa hii usisite kumjulisha na Mwenzio ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza

Imetolewa

ALLY NGALA
Katibu Mkuu IRFA

Viongozi Yanga watua Iringa kuongeza nguvu

Viongozi wapya wa klabu ya Yanga wametimiza ahadi baada ya kuwasili mkoani Iringa kuiunga mkono timu yao inayoshuka uwanja wa Samora kuikabili Lipuli Fc katika mchezo wa nusu fainali kombe la FA

Msafara wa viongozi hao umeongozwa na Mwenyekiti Dk Mbette Mshindo Msolla na Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji

Yanga imeweka mkazo katika kuhakikisha wanatinga fainali na baadae kutwaa taji la kombe la FA ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao

Yanga kuikabili Lipuli Fc ikiwa na mzuka wa kutosha

Yanga iko mkoani Iringa ambapo leo jioni itashuka uwanja wa Samora kuikabili Lipuli Fc katika mchezo wa nusu fainali kombe la FA (ASFC)

Habari njema kwa wachezaji wa Yanga ni kuwa leo watashuka dimbani wakiwa na sapoti ya viongozi wao wapya waliopatikana baada ya uchaguzi jana

Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela anatarajiwa kuwepo uwanjani leo kuwaunga mkono wachezaji kuhakikisha wanashinda mchezo huo

Jana baada ya zoezi la uchaguzi kumalizika, Mwakalebela alisema ataondoka jijini Dar es salaam usiku huo kuwahi mchezo

“Mimi na wenzangu wachache tunaondoka usiku huu kuelekea Iringa kwenda kuwaunga mkono wachezaji wetu. Tunahitaji kushinda mchezo dhidi ya Lipuli ili tuingie fainali”

“Lengo letu ni kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, tunahitaji kutwaa kombe la FA”

Aidha fedha taslim zaidi ya Mil 20 zilichangishwa na Wanachama wa Yanga jana ili kuipa motisha timu kuelekea mchezo huo

Yanga inahitaji kukomaa na kombe la FA ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao

Simba mwendo mdundo, ubingwa huoooo

Ni suala la muda tu kabla ya mabingwa wa nchi, Simba kutangazwa tena kuwa wameuhifadhi ubingwa wao kwa msimu wa pili mfululizo baada ya ushindi wa leo wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons

Simba imejiweka katika mazingira mzuri ya kutetea ubingwa wake baada ya kuondoka na alama zote sita mkoani Mbeya

Mbeya City na Tanzania Prisons zilikuwa zikiangaliwa kuwa na uwezo wa ‘kuitibulia’ Simba hesabu zake kuelekea ubingwa

Simba imesalia na michezo nane, michezo sita itapigwa jijini Dar es salaam kunako uwanja wa Taifa au Uhuru

Simba itatoka nje ya jiji kuzifuata Singida United na Mtibwa Sugar (mchezo wa pili) wakati Coastal Union, Kagera Sugar, Azam Fc, Mtibwa Sugar(mchezo wa kwanza), Ndanda na Biashara United zote zitaifuata Simba ‘majinjioni’ uwanja wa Taifa

Simba huenda ikarejea rasmi kileleni mwa msimamo wa ligi Jumatano May 08 itakapocheza na Coastal Union mchezo utakaopigwa uwanja wa Taifa/Uhuru

FT : Prisons 0-1 Simba

Simba imeendelea kuukaribia ubingwa wa pili mfululizo baada ya leo kuichapa Tanzania Prisons bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya

Bao pekee la Simba lilipatikana kwenye kipindi cha kwanza likiwekwa kambani na Emmanuel Okwi katika dakika ya 11 baada ya shambulizi la kushitukiza

Ushindi huo umeendelea kuisogeza Simba kileleni baada ya kufikisha alama 78 sasa ikihitaji alama mbili tu kuweza kuifikia Yanga

Yanga ina alama 80 ikiwa imecheza michezo minne zaidi ya Simba pia

Okwi ameendelea kuwasogelea vinara wa mabao leo akifikisha mabao 11

Mchezo unaofuata ni dhidi ya Coastal Union na utapigwa May 08 kwenye uwanja wa Taifa