Simba vs Mbao Fc uwanja wa Jamhuri leo

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo Jumapili wanashuka katika uwanja wa Jamhuri kuikabili Mbao Fc katika mchezo wa ligi utakaopigwa saa kumi kamili jioni

Simba iko mkoani Morogoro tangu juzi ikiendelea na maandalizi ya mchezo huo ambao umevuta hisia za mashabiki wa soka mkoani Morogoro na maeneo ya jirani

Kikosi cha Simba kimepania kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Mbao Fc ambayo ilifanikiwa kushinda mchezo wa duru ya kwanza uliopigwa mwaka jana jijini Mwanza

Simba inafukuzia rekodi mpya ya kushinda michezo 10 mfululizo kwenye ligi kuu ya Tanzania Bara

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo na ana matumaini makubwa kuwa wataibuka na ushindi

Ushindi utazidi kuisogeza Simba karibu ya timu zilizo juu yake, Azam Fc na Yanga

Simba yenye michezo 10 ya viporo, inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 54, Azam Fc ina alama 59 ikiwa nafasi ya pili na Yanga bado iko kileleni ikiwa na alama 67

Hata hivyo Simba inaweza kuzipiku timu hizo kama itashinda michezo yake yote ya viporo

Bocco, Kagere kuongoza maangamizi ya Mbao Fc leo

Nahodha wa kikosi cha Simba John Bocco ‘Adebayor’ yuko kwenye kiwango bora sana, leo anatarajiwa kuwaongoza mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara kuikabili Mbao Fc mkoani Morogoro

Baada ya kufanya kazi kubwa ya kuivusha Simba hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa dhidi ya AS Vita, kisha akaivusha Stars fainali za AFCON 2019 katika mchezo dhidi ya Uganda kwa kutengeneza mabao mawili kati ya matatu yaliyofungwa na Stars, Bocco leo atakuwa dimbani kufanya kazi maalum ya kuitafutia Simba alama tatu muhimu

Aidha kinara wa upachikaji mabao katika kikosi cha Simba, Meddie Kagere naye atakuwa na nafasi ya kuongeza mabao yake na kumkaribia Salum Aiyee wa Mwadui Fc mwenye mabao 16

Kagere yuko nafasi ya pili kwenye orodha ya vinara wa upachikaji mabao akiwa na mabao 13

Bocco na Kagere wamerejea kikosini baada ya kutumikia timu zao za Taifa wakiwa ‘fit’ na hakuna shaka Aussems anazihitaji silaha hizi kuweza kuimaliza Mbao Fc baadae leo

Kikosincha Yanga vs Alliance FC

1. Klaus Kindoki

2. Paulo Godfrey

3. Gustavo Simon

4. Said Juma

5. Kelvin Yondani

6. Feisal Salum

7. Mrisho Ngasa

8. Papi Tshishimbi

9. Heritier Makambo

10. Amissi Tambwe

11. Pius Buswita

SUB

Ibrahim Hamid

Jaffar Mohammed

Andrew Vicent

Haruna Moshi

Thabani Kamusoko

Raphael Daudi

Deus Kaseke

Zahera awafungulia mlango wanaotaka ‘kusepa’

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema amezisikia tetesi zinazowahusu wachezaji wake wanaowaniwa na timu nyingine na ametoa ruhusa kwa mchezaji yeyote anayetaka kuondoka, aondoke

Zahera ambaye yuko Mwanza na kikosi cha Yanga ambacho leo kinatarajiwa kushuka uwanja wa CCM Kirumba kuumana na Alliance Fc katika mchezo wa robo fainali kombe la FA, amesema hana wasiwasi kama wachezaji hao wataondoka kwa kuwa amedhamiria kuisuka upya Yanga kwa ajili ya msimu ujao

Aidha Zahera amesema Yanga ya sasa sio tegemezi, haiwezi kutetereka kama wachezaji hao wataondoka hata leo

“Watu wananipigia simu kuniuliza kuhusu wachezaji wa Yanga hasa Yondani, Tshishimbi, Ajibu na Feisal kutakiwa na timu nyingine.”

“Tangu mwanzo wa ligi ukiangalia kuna mechi mingi tulizocheza, angalia mechi ngapi tuilicheza bila Kevin ngapi tulicheza bila Tshishimbi bila Ajibu na Feisal. Kuna mechi tulicheza bila watatu kati yao ndani ya mechi moja na tulishinda,” amesema Zahera

“Nikisikia leo Yanga hakuna mchezaji hata mmoja kwenye timu ninaweza kulia lakini mchezaji mmoja akikosa siwezi kukosa usingizi.”

“Mchezaji yeyote anayetaka kuondoka anaweza kuondoka, hakuna hata mchezaji mmoja anaweza kuniogopesha kwakuwa timu fulani inamtaka lakini najua msimu ujao wa ligi timu hii itabadilika sana.”

“Yanga sio team ya mchezo, Yanga ni timu kubwa na inawachezaji wakubwa. Yanga ina wachezaji wazuri lakini msimu unaokuja nadhani Yanga itakuwa na wachezaji wakubwa saana.”

Robo fainali ya tatu kombe la FA kupigwa leo, Yanga kesho

Michuano ya kombe la FA (ASFC) hatua ya robo fainali inaendelea leo kwa mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam FC utakaopigwa uwanja Kaitaba

Huo utakuwa mchezo wa tatu wa robo fainali baada ya juzi kuzishuhudia Lipuli Fc na KMC kutinga nusu fainali baada ya kushinda michezo yao

Kesho Jumamosi Yanga itakamilisha hatua hiyo ya robo fainali kwa kuumana na Alliance Fc katika mchezo utakaopigwa dimba la CCM Kirumba

Mshindi wa mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Azam Fc atachuana na KMC kwenye mchezo wa nusu fainali wakati mshindi wa mchezo wa kesho kati ya Alliance Fc dhidi ya Yanga, ataumana na Lipuli Fc kwenye mchezo wa nusu fainali

Simba yaifuata Mbao Fc Morogoro

Msafara wa kikosi cha Simba umeondoka jijini Dar es salaam asubuhi ya leo Ijumaa, kuelekea Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC ambao utapigwa siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Jamhuri

Leo jioni Simba inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya kwanza katika uwanja wa Jamhuri ambao uongozi wa timu hiyo uliufanyia ukarabati wa sehemu ya kuchezea ‘pitch’

Baada ya mchezo dhidi ya Mbao Fc, Simba itaendelea kubaki mkoani Morogoro kuendelea na maandalizi ya mchezo wa robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe