Afisa Habari wa Yanga Dismas Ten amewataka mashabiki wa Simba wavumilie ‘madongo’ wanayovurumishiwa baada ya jana kufumuliwa mabao 4-1 na TP Mazembe na kuondoshwa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika hatua ya robo fainali
Kutupwa nje ya michuano hiyo kwa Simba kuliibua shangwe kubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga na hii inatokana na Simba kutumia mafanikio yao msimu huu ‘kuwanyanyasa’ watani zao Yanga ambao wanapita katika kipindi kigumu
Ten amesema Yanga na Simba ni watani wa jadi hivyo ni vyema wakavumilia matani wanayokutana nayo mtaani kwani na wao wamekuwa wakifanya hivyo wakati wote ambao Yanga inakumbwa na changamoto
“Ndiyo Sisi na ninyi ni watani na tunataniana kweli hasa timu zetu zinapokosa matokeo,” ameandika Ten kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram
“Bahati mbaya ni kwamba ninyi mnapenda kutania wenzenu lakini mkitaniwa ninyi ‘Nongwa’ mnahamia kwenye kashfa..! Mkikashifiwa nanyi mnaanza kulialia”
“Hongereni kwa hatua mliyofika, muhimu ni kuangalia wapi mmekosea ili mfanikiwe zaidi siku za usoni”
“Wakati sisi tunajiuliza nanyi mjiulize zaidi. Msimvuruge @moodewji ili aendelee kuwabeba..!”
Aidha Ten amewakaribisha Simba kwenye ligi kuu huku akiwatupia ‘dongo’ kuwa mitandao yao ya simu itakuwa imejaa tayari kwa kufanya miamala
“La huko limeisha, mrudi bongo sasa najua simu zenu zina line mbili mbili yaani full network kama siyo Mpesa basi Tigopesa…!”
Baada ya kutolewa Simba inarejea kwenye ligi ikikumbana na rundo la ‘viporo’ ambavyo watatakiwa wavimalize ndani ya kipindi cha mwezi mmoja
Katika kipindi hicho Simba wanapaswa kucheza michezo 16 kwani ligi imepangwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa tano ili kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ambayo mwezi Juni inaelekea Misri kushiriki fainali za AFCON 2019