Michezo 12 kuamua hatma ya ubingwa Yanga

Kimahesabu Yanga bado inayo nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kama itachanga vyema karata zake

Michezo 12 iliyosalia inaweza kuipa Yanga alama 36 na kuwafanya mabingwa hao wa kihistoria kuweza kufikisha alama 100

Habari njema kwa Yanga ni kuwa haina kibarua kikubwa sana cha michezo ya mikoani ukilinganisha na wapinzani wao katika mbio za ubingwa Simba

Simba iliyoshuka dimbani mara 20 bado ina deni la michezo 18 hivyo kuwafanya bado wawe na kazi kubwa licha ya kuwa na faida ya kimahesabu iwapo wataweza kushinda michezo yao yote

Yanga imebakiza michezo minne tu ya nje ya jiji la Dar es salaam huku michezo nane ikitarajiwa kupigwa uwanja wa Taifa

Michezo ya ugenini ambayo itapigwa nje ya jiji la Dar es salaam ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Lipuli Fc, Ndanda na Biashara wakati michezo dhidi ya Azam Fc na Ruvu Shooting ni ya ugenini lakini itapigwa jijini Dar es salaam

Michezo iliyobaki ambayo Yanga ni mwenyeji ni dhidi ya KMC, African Lyon, Prisons, Mbeya City, Azam Fc na Kagera Sugar

FULL TIME: YANGA 1-0 ALLIANCE FC

Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga wameendelea kujikita kileleni katika msimamo wa ligi baada ya kuichapa Alliance Fc bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa dimba la CCM Kirumba

Ulikuwa ni mchezo wa ushindani kutoka kwa kila upande ambapo kikosi cha Alliance Fc kimeonekana kuimarika sana tofauti na wakati timu hizo zilipokutana kwenye dimba la Taifa mwaka jana

Bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na mshambuliaji mkongwe Amissi Tambwe kwenye dakika ya 75 ya mchezo

Hilo lilikuwa bao la nane kwa Tambwe msimu huu

Katika mchezo huo Heritier Makambo alikosa mkwaju wa penati mapema tu kwenye dakika ya sita baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Matokeo hayo yameifanya Yanga iendelee kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 64

Okwi awasubiri JS Saoura

Mshambuliaji hatari wa Simba Emmanuel Okwi hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoikabili Stand United kesho kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara utakaopigwa katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Okwi alipata majeraha madogo kwenye mchezo dhidi ya Lipuli Fc. Lakini pia Okwi alicheza mchezo huo huku akiwa amefungwa bandeji chini ya jicho kutokana na jeraha la kuchanika alilopata kwenye mchezo dhidi ya Azam Fc

Baada ya mchezo wa Lipuli Fc, Okwi alirejeshwa jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi

Hata hivyo taarifa za uhakika ni kuwa kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amempa mapumziko mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uganda ili aweze kupona kabisa majeraha yake tayari kwa mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Saoura

Baada ya mchezo dhidi ya Stand, Simba itasafiri kwenda Algeria kuikabili JS Saoura kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya makundi, raundi ya tano utakaopigwa Jumamosi ijayo, March 09 2019

Simba inahitaji angalau pointi moja tu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo

Aussems apania kunyamazisha ‘kelele’ za Stand United

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema timu yake imefuata alama tatu mkoani Shinyanga hivyo iko tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Stand United utakaopigwa kesho Jumapili kwenye uwanja wa CCM Kambarage

Simba iliweka kambi ya siku mbili mkoani Singida kabla ya kutua Shinyanga hapo jana

Aussems amesema anatambua mchezo huo hautakuwa mwepesi lakini kama walivyofanya katika michezo iliyopita, lengo lao ni kuondoka na alama zote tatu

Juzi kocha wa Stand United Athuman Bilali ‘Bilo’ alitamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi katika mchezo huo ambapo alisema Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo Ndanda Fc, Mwadui Fc na timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu

“Tumewafuata Stand United, tunajua kila timu sasa inajiandaa kuonyesha ushindani itakapocheza na sisi, tunajua hilo, lakini mipango yangu ni kuhakikisha tunashinda mechi hii ya Jumapili, tuko tayari,” alisema Aussems jana baada ya kutua mkoani Shinyanga

Jana jioni kikosi cha Simba kilijifua mkoani Shinyanga kujiandaa na mchezo huo ambao ushindi utazidi kuisogeza Simba kileleni

Simba kuelekea Shinyanga leo, Okwi arudi Dar

Mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi alipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Lipuli Fc na kulazimika kurejea jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu zaidi

Hata hivyo Okwi bado anaweza kuungana na kikosi cha Simba kwa ajili ya mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa keshokutwa katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema hatma yake itategemea na ripoti ya Daktari wa timu hiyo Dk Yassin Gembe

Wakati huo huo Simba inaondoka mkoani Singida leo kuelekea Shinyanga tayari kwa mchezo dhidi ya Stand United utakaopigwa Jumapili