SIMBA SC: Kuwafata JS Saoura LEO

Leo jioni kikosi kitaondoka kuelekea nchini Algeria kwa kupitia Dubai, UAE ambako kitacheza mchezo wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura, mchezo ambao utachezwa siku ya Jumamosi Machi 9, 2019. Tuikumbuke timu yetu kwenye dua ili ifike salama na ifanye vizuri katika mchezo huo muhimu. #NguvuMoja

KAGERE Atoa NENO Kuelekea SIMBA vs JS SAOURA

Mshambuliaji wa Simba kinara wa mabao Meddie Kagere amewataka mashabiki wote wa mabingwa hao wa Tanzania Bara kuungana kuipa sapoti timu wakati huu inaokabiliwa na mchezo muhimu wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Saoura

Kagere amewataka mashabiki kuiombea na kuiunga mkono timu kwa hali na mali ili kuhakikisha inatinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa

“Nawaambia wote wenye mapenzi mema na Simba, wale wanaoamini kuwa tunaweza kutinga robo fainali, nusu fainali na hata fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, waungane nasi kwa kutuombea ili tuweze kufanikiwa,” amesema Kagera katika ujumbe mfupi alioutuma kwa mashabiki wa Simba

Simba inatarajiwa kwenda Algeria siku chache zijazo tayari kwa mchezo huo dhidi ya JS Saoura utakaopigwa Jumamosi, March 09

Michango yamkatisha tamaa Zahera

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema hataendelea kubaki katika klabu hiyo kama Wana Yanga hawatajitoa kuichangia timu kwa ajili ya mipango ya msimu ujao

Akihojiwa na moja ya redio maarufu nchini, Zahera amesema amekuwa akijitoa kuisaidia Yanga na alitarajia Wana Yanga nao watafanya hivyo wakati huu ambao timu inapita katika kipindi kigumu lakini hali imekuwa tofauti

“Wanasema Yanga ni timu ya Wananchi lakini mbona wananchi hao hawaonekani kuisaidia timu?” alihoji Zahera

“Msimu huu hatukuwa na malengo ya kutwaa ubingwa, sababu iko wazi, kikosi chetu hakijakamilisha mahitaji ya kuweza kuwa mabingwa”

“Nilitegemea Wana Yanga watachangia timu kama tulivyopendekeza ili msimu ujao tuweze kuwa na kikosi imara zaidi”

“Lakini kwa hali inavyoendelea mimi sitakuwa tayari kufanya kazi kwenye timu ambayo haina malengo.”

“Sitakuwa tayari kuendelea kuwasaidia watu ambao wenyewe hawajisaidii”

Zahera amefanya kazi kubwa msimu huu ambapo licha ya mapungufu yaliyopo, ameweza kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ikipoteza michezo miwili tu

Kocha huyo Mcongomani anataka kuiona Yanga inatoka katika ‘ukata’.

Pendekezo la kuwataka Wana Yanga waichangie timu yao ni moja ya njia za muda mfupi zinazoweza kuifanya Yanga ikasimama wakati ikiendelea kuandaa mikakati ya kuweza kujitegemea kama walivyo watani zao Simba

Hata hivyo muitikio mdogo wa Wana Yanga katika kutoa michango umemfanya kocha huyo akate tamaa na pengine huenda akaondoka mwishoni mwa msimu kama mambo hayatabadilika

Wadau wapendekeza Harambee ya kuichangia Yanga

Ili kuongeza kasi ya uchangiaji wa klabu ya Yanga, baadhi ya wadau wamependekeza uongozi wa Yanga uandae ‘Harambee’ ambayo itakuwa ni siku maalumu kwa Wana Yanga kuichangia timu yao

Harambee hiyo inaweza kuandaliwa na kufanyika katika ukumbi utakaofaa ambapo utaratibu wa kutoa mwaliko kwa wadau wa Yanga unaweza kuandaliwa

Hapa waalikwe wananchi wa kawaida, watu maarufu, wafanyabishara, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali kiufupi Yanga ina mtaji mkubwa wa watu, siku hiyo inaweza kutumika kuwaunganisha watu wote

Pia unaweza kuandaliwa utaratibu kwa tukio hilo kurushwa ‘mbashara’ katika runinga na redio mbalimbali ili wadau wengine ambao hawakualikwa waweze kushiriki kwenye Harambee hiyo kupitia vyombo vyao vya habari

Uchangiaji utafanyika ukumbini kwa kuwashirikisha wadau walioalikwa huku pia namba za kuchangia zikiendelea kutangazwa kwa wale wanaofuatilia kupitia vyombo vya habari ili waweze kuchangia

Utaratibu huu sio mgeni umekuwa ukitumiwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali katika kuzishirikisha jamii zao linapokuja suala la uchangiaji wa fedha

RUGE KUPUMZISHWA LEO

Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Vipindi Clouds Media, Ruge Mutahaba unatarajiwa kuzikwa leo katika kijiji cha Kisiru Wilayani Bukoba mkoa wa Kagera

Baada ya kuagwa jijini Dar es salaam, mwili wa Ruge ulisafirishwa jana Jumapili kuelekea Bukoba tayari kwa mazishi hayo

Wananchi wengi walijitokeza uwanja wa Ndege wa Bukoba katika mapokezi ya mwili wa Ruge ambaye enzi za uhai wake alikuwa mtu wa watu

Watu wengi wamesafiri kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kwenda kumzika Ruge

Kabla ya ibada ya mazishi jioni ya leo, mwili wa Ruge utaagwa kwenye viwanja vya Ghymkhana kijijini Kiziru

Kagere apania kumpiku Aiyee

Licha ya Mwadui Fc kubamizwa mabao 6-2 na Ruvu Shooting jana, mshambuliaji wa timu hiyo Salim Aiyee alifunga moja ya mabao na kumfanya afikishe mabao 14

Leo Meddie Kagere anatarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Simba kwenye mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Stand United utakaopigwa uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga

Kagere mwenye mabao 12, yuko katika kiwango bora cha upachikaji mabao, akifunga mfululizo kwenye michezo mitano iliyopita

“Kazi yangu mimi ni kufunga, hivyo nitaendelea kufanya hivyo kila ninapopata nafasi ili niisaidie timu yangu iweze kupata ushindi,” alisema Kagere baada ya mazoezi ya jana

Kagere ndiye mchezaji hatari zaidi katika ligi kuu ya Tanzania Bara kwa sasa kutokana na kuwa na wastani mzuri wa kufunga kulingana na uwiano wa michezo aliyocheza