Ronaldo ni Habari Nyingine Aipiga Atletico Hat Trick

Ronaldo ni Habari Nyingine Aipiga Atletico Hat Trick

DUNIA nzima inatambua ubora wa mshambuliaji wa Juventus, Cristiano Ronaldo na hakuna ambaye alishangaa kwa kile alichofanya usiku wa kuamkia leo kwenye Dimba la Allianz nchini Italia.

Juventus kwenye mchezo wa kwanza waliocheza nchini Hispania wiki tatu zilizopita walichapwa mabao 2-0 na Atletico Madrid katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini jana Ronaldo alipiga mabao matatu ‘hat trick’ na kuipeleka Juventus robo fainali.

Ronaldo ambaye ameshatwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia mara tano, alifunga mabao hayo kila kipindi na kuipa timu yake ushindi wa mabao 3-0, ikatinga robo fainali kibabe.

Ronaldo ambaye ameshatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne, alifunga mabao yake yote mawili ya kwanza kwa kichwa, alifunga la kwanza katika dakika ya 27 na bao la pili katika dakika ya 48 ya mchezo huo.

Hata hivyo, wakati Atletico wakipambana kurudisha, Juventus walipata penalti dakika ya 86 ambapo Ronaldo alichukua mpira na kuweka kimiani bao la tatu kwa timu yake na yeye akiondoka na mpira usiku huo baada ya kufunga hat-trick yake ya kwanza msimu huu kwenye Uefa na kuwafanya wafuzu kwa jumla ya mabao 3-2.

Huu ndiye mchezo wa kwanza ambao Ronaldo ameonyesha Kiwango cha hali ya juu sana msimu huu kuanzia alipojiunga na Juventus mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Real Madrid.

Hii ni picha halisi kuwa staa huyo anaweza kutwaa tena tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwakani.

MAN CITY NAO WAFUZU

Manchester City ambao wamekuwa wakiutafuta ubingwa huu kwa muda mrefu bila mafanikio jana walifanikiwa kufuzu kwenda robo fainali baada ya kuwachapa Wajerumani, Schalke 04, mabao 7-0.

Awali City walishinda kwa mabao 3-2 ugenini, lakini jana wakiwa nyumbani kwenye Dimba la Etihad, walionyesha kiwango cha hali ya juu na kupata ushindi huo mnono.

Sergio kun Aguero alikuwa shujaa kwenye timu hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika ya 35 kwa mkwaju wa penalti na 38.

Mabao mengine ya City ambao wanaongoza kwenye Ligi Kuu England yaliwekwa kimiani na Sané (43), Sterling (56), Bernardo Silva dakika ya 71, Foden aliyefunga la sita dakika ya 78 na Jesus akafunga kitabu dakika ya 84 na kuwafanya City wafuzu kwa jumla ya mabao 10-2.

City imekuwa timu ya kwanza kupata ushindi mnono zaidi kwenye hatua ya 16 Bora msimu huu. Sasa inamaana kuwa City imeungana na Ajax, Manchester United, Juventus, Porto na Tottenham kwenda hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.

SABABU Za AJIBU Kuanzia BENCHI

Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amewataka wanaohoji kwa nini nahodha wa kikosi cha timu hiyo Ibrahim Ajib haanzi katika michezo ya hivi karibuni kuwa watulie kwani yeye ndiye anayefahamu mahitaji ya kila mechi

Katika mahojiano na Radio UFM, Zahera amesema huwa anapanga kikosi chake kufuatana na mahitaji ya mpinzani anayekutana nae

“Kwa wanaofuatilia wanafahamu, sio Ajib tu ambaye huwa anapumzika, nimekuwa nikibadili wachezaji mara kwa mara kufuatana na mahitaji ya mchezo,” alisema Zahera

“Mabadiliko haya ni ya kawaida, haimaanishi kwamba Ajib kashuka kiwango au nina ugomvi nae”

“Wapo watu ambao kazi yao ni kufanya uchonganishi Yanga, nawashauri wafanye mambo mengine yenye faida kwao”

Baada ya kuwa na mwenendo mzuri tangu akabidhiwe kitambaa cha unahodha, Ajib amehusika kwa kucheza michezo mingi ya Yanga kabla ya michezo mitatu iliyopita ambayo yote hakuanza

Ajib amefunga mabao sita msimu huu na kutoa pasi za mabao 15.

Mpaka sasa ndiye mchezaji mwenye mafanikio zaidi kwenye ligi kwani kati ya mabao 45 ayliyofungwa na Yanga, Ajib amehusika katika mabao 21

SIMBA SC Yatua DAR

Makamanda wetu wamewasili nchini salama. Jumamosi watakuwa Uwanja wa Taifa kutoa burudani kwa Wanasimba na Watanzania wote. Hii ni #DoOrDie #NguvuMoja ✊🏽

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama, tuna mchezo mwingine tutacheza na AS Vita, mimi naamini kabisa kwa morali tuliyonayo na mbinu za kocha tukiwepo nyumbani tutapambana na tutafuzu”- Nahodha John Bocco baada ya kuwasili nyumbani 🇹🇿. #DoOrDie #NguvuMoja ✊🏽

MO DEWJI: Tukutane Taifa

Mwekezaji wa klabu ya Simba Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ amewataka mashabiki wa timu hiyo na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo wataki Simba itakapochuana na Vita Club

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Mo amesema kwa sasa hapendi kuzungumza maneno mengi lakini anawaita uwanja wa Taifa mashabiki wa Simba Watanzania wote kuiunga mkono Simba katika mchezo huo muhimu

“Sina maneno mengi, tukutane uwanjani wanaSimba na waTanzania wote kwa ujumla,” ameandika Mo

Katika michezo yote msimu huu ambayo Mo yuko uwanjani, Simba imeibuka na ushindi.

Licha ya kuwa mwekezaji, Mo amejipambanua kuwa shabiki na muhamasishaji namba moja wa klabu ya Simba kuelekea ‘gemu’ kubwa