Dk Msolla Atangaza kusaka kocha msaidizi – YANGA

Habari njema kwa Wanajangwani ni kuwa uongozi wa Yanga umetangaza kuanza mchakato wa kutafuta kocha Msaidizi Mzawa ambaye atasaidiana na kocha Mwinyi Zahera kukinoa kikosi cha Yanga

Tangu alipoanza kazi mwishoni mwa msimu uliopita, kocha Zahera hakuwa na Msaidizi zaidi ya Noel Mwandila ambaye amekuwa akikaimu nafasi hiyo licha ya kuajiriwa Yanga kama kocha mtaalamu wa viungo

Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshondo Msolla ambaye kitaalam ni kocha, amesema kuna umuhimu kwa benchi la Ufundi kuongezewa nguvu kwa kuajiri kocha Msaidizi mzawa ambaye atakuwa sambamba na Zahera

“Benchi la ufundi linahitaji kuwa na kocha msaidizi mwenye kiwango kizuri ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi chetu, tutaangalia zaidi kocha mzawa ili aweze kuwa sambamba na kocha Zahera kufanya kazi,” amesema

SIMBA 2-0 NDANDA FC

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba wanahesabu siku za kukabidhiwa ubingwa wa pili mfululizo baada ya leo kuichapa Ndanda Fc mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Uhuru

Wakicheza kandanda la pasi fupifupi lililojaa ufundi wa hapa na pale, Simba ilijipatia mabao yake yote mawili kwenye kipindi cha kwanza yote yakiwekwa kambani na Meddie Kagere ‘MK14’

Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama 88 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tano dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 83

Yanga imebaki na michezo miwili, inahitaji kushinda yote ili kuweza kuipiku Simba lakini wakati huohuo Simba bado ina michezo mitatu mkononi

Ni muujiza pekee ambao utaifanya Simba isiweze kutwaa ubingwa!

Aidha Simba inaweza kwenda kumaliza ‘shughuli’ mkoani Singida keshokutwa itakapoivaa Singida United

Kwenye mchezo huo Simba inahitaji alama moja tu kuweza kurejea na ubingwa jijini Dar es salaam

Kinara wa mabao Meddei Kagere amezidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha dhahabu baada ya leo kufikisha mabao 22

Kagere anaongoza kwa tofauti ya mabao sita dhidi ya Heritier Makambo na SalimAiyee ambao wote wana mabao 16

AISHI MANULA Aipania SEVILLA

Mlinda lango wa Simba Aishi Manula amesema mchezo dhidi ya Sevilla una maana kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo kwani watakuwa na nafasi ya kuonyeshwa ukubwa wa timu yao

“Simba kucheza na Sevilla ndani ya uwanja wa Taifa ni jambo kubwa sana,” amesema

“Kwetu sisi wachezaji ni nafasi kubwa sana kuonyesha ubora wetu na kutimiza malengo ya timu yetu ambayo ni kufanya vizuri Kimataifa”

“Nawaalika mashabiki waje kwa wingi uwanja wa Taifa May 23 kuipa sapoti SImba, kuipa sapoti Tanzania”

Simba na Sevilla zitachuana Alhamisi, May 23 katika mchezo wa ‘kukata na shoka’ utakaopigwa uwanja wa Taifa kuanzia saa moja kamili jioni

Cristiano Ronaldo ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu nchini Italia “Serie A” kwa msimu 2018/19

✍🏼 Mshambuliaji wa Klabu ya Juventus, Cristiano Ronaldo ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu nchini Italia “Serie A” kwa msimu 2018/19, Cr7 ametwaa tuzo hii ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu kusakata soka nchini Italia.
:
✍🏼 Ronaldo alikuwa sehemu ya kikosi cha Vibibi hivyo vya Turin kwenye kutwaa Scudetto yao ya nane mfululizo huku Cr7 ikiwa ni ya kwanza kwake na yeye mwenyewe akipachika Mabao yake 21 katika Ligi. Tuzo za Serie A kila mshindi anapewa baada ya kumalizika kwa msimu, lakini Ronaldo atapewa tuzo yake kabla ya mchezo wao dhidi ya Atalanta siku ya leo Jumapili.
:
✍🏼 Wachezaji wengine waliotwaa tuzo katika Ligi hiyo ni, Mlinda lango Bora wa Msimu katokea Inter Milan, Samir Handanovic, Beki Bora wa Msimu imebebwa na Muafrika kutoka Senegal, Kalidou Koulibaly anaekipiga Napoli, Kiungo Bora Ligi Kuu Italia imebebwa na fundi wa kumiliki Dimba La Kati, Sergej Milinkovic-Savic kutoka Klabu ya Lazio, Fabio Quagliarella Mshambuliaji hatari wa Sampdoria kabeba tuzo ya Mshambuliaji bora wa msimu na Nicolo Zaniola kinda ambaye anacheza Klabu ya AS Roma, yeye kaibuka Mchezaji bora kijana wa Mwaka ndani ya Serie A.
:
✍🏼 Ronaldo Sasa katwaa tuzo ya Mchezaji bora wa mwaka Italia, England na Hispania pamoja na kutwaa Ubingwa wa Ligi kwa nchi zote tatu.. Koulibaly amekuwa nguzo ya ulinzi ndani ya Napoli blocks 31, Clearance 125, tackles won 60 Kati ya 67, clean sheets 13 katika mechi 31 alizocheza..
#seriea #juventus #napoli #lazio #asroma
@Sokawaytz

HARUNA NIYONZIMA NI MZURI KULIKO CHAMA – Mwl KASHASHA

Mwalimu kashasha katika Sehemu ya tanoya Uchambuzi wake
@mwalimu_alex_kashasha

Mchambuzi wa soka Nchini Tanzania Mwalimu Kashasha amesema kuwa watanzania wakua chanzo cha wachezaji wengi kucheza na Majukwaa

Huku akimsfia niyonzima kuwa hatakama anacheza na Majukwaa ila bado anaspeed katika mpira wake, kashasha amesema kwake yeye Haruna ni Mzuri kuliko chama

Anasema kuwa Haruna Kwa sasa amebadilila na amkua msaada kwa timu kutokan na Uchezaji wake

Usikose Mwendelezo wa Uchambuzi wa Mwalimu kashasha katika Sehemu ya Sita.

Powered By @bikotanzania
Imeandaliwa na @officialchristz video kwa hisani ya @globalpublishers

ZAHERA APEWA MAJUKUMU HAYA YANGA

Katika kuhakikisha timu zote za Yanga zinakuwa imara, uongozi wa timu hiyo umemtangaza Mwinyi Zahera kuwa msimamizi Mkuu wa timu zote

Akizungumza kwenye hafla ya Iftar Gala Dinner iliyofanyika Hotel ya Serena jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema Zahera ambaye ni kocha wa kikosi cha kwanza, pia atasimamia timu ya Vijana (Yanga B) na timu ya Wanawake (Yanga Princess)

“Kwa sababu ya masuala ya ufundi, natangaza mbele yenu, timu zote zitakuwa chini ya kocha Mwinyi Zahera,” alisema Dk Msolla

“Ni lazima kama timu tuwe na filosofia moja. Hivyo tumeona filosofia inayotumiwa kwenye kikosi cha kwanza ni lazima ikafuatwa na makundi yote. Zahera atakuwa msimamizi Mkuu”

ASISITIZA KUVUNJWA MAKUNDI

Dk Msolla amewataka Wanayanga kudumisha umoja ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea

Aidha amesema ahadi walizotoa wakati wa kampeni watazitimiza ambapo ameahidi kushirikiana na waliokuwa wagombea wengine wa nafasi mbalimbali lakini bahati mbaya kura hazikutosha

“La kwanza lilikuwa kuleta mshikamano na kuirudisha timu kwa Wananchi”

“La pili lilikuwa kubadilisha mfumo na uendeshaji wa timu. Nawaahidi mbele yenu hili tutalifanya ndani ya mwaka mmoja au chini ya hapo”

“La tatu muhimu tutasaidia miradi inayoendelea klabuni sasa ambayo ni ujenzi wa uwanja, ukarabati wa jengo na miradi mipya”

“Nafurahi Igangula hapa amesema yuko tayari kutoa ushirikiano, niliona randama yake wakati wa kampeni, nawaahidi tutashirikiana nae na tutahakikisha atakuwa sehemu ya uongozi wetu”

“Dk Tiboroha ameshindwa kufika hapa kutokana na kuchelewa kutoka safarini Arusha lakini ameahidi kuchangia Tsh Milioni Moja kwa ajili ya shughuli mbalimbali za klabu, na yeye tuko nae pamoja”

“Muhimu nimeomba sote tuvunje makundi yetu baada ya uchaguzi. Umoja na Ushirikiano wetu utatusaidia kusonga mbele kwa haraka”

UTAWALA BORA

Dk Msolla amesema katika uongozi wake watahakikisha wanafuata utawala bora na watakuwa makini katika usimamizi wa fedha

“Maeneo ya ukaguzi wa ndani na nje tutakuwa wakali sana. Tutakuwa tayari kutumia gharama kuwapata wakaguzi wanaoheshimika Kimataifa na tutakuwa tukitoa ripoti wazi kwenye vyombo vya habari kuhusu mapato na matumizi ya klabu kama zinavyofanya taasisi nyingine”

KUIMARISHA KIKOSI CHA YANGA

Dk Msolla amesema kwa ushirikiano ulioonyeshwa na makundi mbalimbali ya Yanga, ndani ya wiki mbili au tatu, zoezi la kukiboresha kikosi litakuwa limeanza

“Nawaahidi ndani ya wiki mbili au tatu zijazo, tutaanza kutengeneza kikosi imara chini ya usimamizi wa kocha Mwinyi Zahera”

SIMBA Kusaka Ushindi Leo Dhidi ya Ndanda FC

Mabingwa watetezi ligi kuu ya Tanzania Bara Simba leo wanashuka uwanja wa Uhuru kuikabili Ndanda Fc katika mchezo ambao matokeo ya ushindi yataisogeza Simba karibu ya ubingwa wa pili mfululizo

Simba inayoongoza ligi ikiwa na alama 85, inahitaji alama nne tu kutetea ubingwa kwa msimu wa pili

Kuhakikisha alama tatu zinapatikana leo, kikosi cha Simba kiliingia kambini juzi baada ya kufanya kikao na Mwekezaji wa klabu hiyo Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’

Hesabu za kocha Patrick Aussems ni kuhakikisha wanashinda mchezo wa leo na ule utakaofuata dhidi ya Singida United ili kujihakikishia ubingwa kabla ya mechi mbili za mwisho

Baada ya mchezo leo, Simba itaondoka jijini Dar es salaam kuelekea Singida ambako keshokutwa Jumanne, May 21 itacheza na Singida United

May 22 Simba itafunga safari kurejea jijini Dar es salaam ambapo May 23 inakabiliwa na mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sevilla

Sevilla inatarajiwa kuwasili keshokutwa tayari kwa mchezo huo ambao utalipaisha jina la Simba na Tanzania Kimataifa kwani utarushwa ‘mbashara’ na vituo vikubwa vya runinga duniani

Kuelekea mchezo wa leo, Meneja wa Simba Patrick Rweyemamu amesema wachezaji wa timu hiyo wako tayari, wanafahamu Wanamsimbazi wanahitaji ushindi