Michuano Ya Sportpesa kufanyika January 2019

Michuano ya SportPesa Super Cup inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa inatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia January 22 hadi January 27 2019.

Michezo hiyo inatarajiwa kupigwa dimba la Uhuru na CCM Kirumba.

Akizungumza na waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Hostel za Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Mkurugenzi mtendaji wa SportPesa Tarimba Abas amesema timu nane zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo.

Timu hizo ni Simba, Yanga, Singida United FC na Mbao FC zote kutoka Tanzania huku upande wa Kenya ni Gor Mahia, AFC Leopards, Bandari na Kariobangi Sharks.

Tarimba amesema Mbao Fc imealikwa kwenye michuano hiyo ya tatu kutokana na Klabu hiyo kuonyesha ushindani mkali katika Ligi kuu ya Tanzania Bara.

Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia kitita cha dola 30,000 pamoja na kukata tiketi ya kwenda nchini Uingereza kucheza na Everton Fc

TFF yawafungia Mwenyekiti, Katibu Matawi Yanga Sc

Kamati ya maadili ya Shirikisho la soka nchini (TFF) inayoongozwa na Mwenyekiti Hamidu Mbwezeleni imemfungia Mwenyekiti wa matawi wa klabu ya Yanga Bakili Makele na katibu wa matawi wa klabu hiyo Boaz Ikupilika kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miaka mitatu.

Viongozi hao pia wametakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 2 kila mmoja kwa kukaidi maamuzi ya serikali na TFF yanayohusiana na maagizo ya kufanyika uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo ziko wazi ndani ya klabu ya Yanga.

Viongozi hao walihojiwa na kamati ya maadili hivi karibuni wakituhumiwa kupinga mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Yanga ulioandaliwa na TFF kwa maagizo ya BMT.

TFF ilivyokosa Msimamo kwa nafasi ya MANJI yanga Sc

Julai 11 2018 Shirikisho la soka nchini (TFF) lilimuondoa kwenye nafasi yake aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Clement Sanga baada ya kupokea barua kutoka kwa uongozi wa Yanga ikimtambulisha Yusufu Manji kuwa amerejea klabuni hapo.

Sanga aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga alipoteza sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi baada ya TFF kuikubali barua ya Yanga iliyomtambulisha Manji kuwa Mwenyekiti baada ya kuridhia kurejea.

Sifa ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu ni lazima uwe Mwenyekiti wa timu inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo uamuzi huo uliotolewa miezi minne iliyopita na TFF ni kinyume kabisa na uamuzi wao wa sasa wa kuitaka Yanga ifanye uchaguzi wa kujaza nafasi ya Manji licha ya kuwa tayari walishamtambua na uamuzi wao huo ulisababisha Sanga akapoteza kibarua chake kwenye Bodi ya Ligi.

Inafahamika uamuzi wa sasa umetolewa na BMT na TFF ni watekelezaji tu lakini ni wazi TFF imeonyesha kutokuwa na msimamo katika jambo hili la uchaguzi wa Yanga hasa kwenye nafasi ya Mwenyekiti

Lwandamina Amtaka Tshishimbi ZESCO

Baadhi ya magazeti nchini Zambia yameripoti kuwa klabu ya ZESCO United itamsajili kiungo wa Yanga Papi Tshishimbi mwishoni mwa msimu.

ZESCO inanolewa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina aliyejiunga na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita.

Mkataba wa Tshishimbi wa kuitumikia Yanga unamalizika mwishoni mwa msimu huu kama Yanga itashindwa kumshawishi asaini mkataba mpya basi huenda akaenda kujiunga na timu hiyo akiwa mchezaji huru.

Alipotua Yanga msimu uliopita akitokea Mbabane Swallows, Tshishimbi alionyesha kiwango cha hali ya juu.

Hata hivyo msimu huu bado haujawa mzuri sana kwake kutokana na kukabiliwa na majeruhi ya mara kwa mara. Ameshindwa kufikia makali yake ya msimu uliopita

Mzee Akilimali Apinga MANJI Kurudi Yanga

Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga Ibrahim Akilimali amepinga kurejea kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusufu Manji na ameitilia shaka barua inayodaiwa kuwa ameiandika kuridhia kurejea katika nafasi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Akilimali ambaye tayari amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Uwenyekiti ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iichunguze barua hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Kapteni George Mkuchika.

Aidha Akilimali amedai kushangazwa na viongozi wa Yanga kuendelea kumsemea Manji wakati yeye mwenyewe yupo.

Akilimali amemtaka Manji ajitokeze hadharani kuwaambia WanaYanga kama amerejea au la na sio kusemewa na watu wengine kila siku.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti kamati ya Uchaguzi ya TFF Malange Mchungahela amewataka viongozi wa Baraza la Wadhamini Yanga pamoja na wajumbe Kamati ya Utendaji wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua kutokana na kutaka kuvuruga mchakato wa Uchaguzi wa klabu hiyo.

Mchungahela amesisitiza kuwa zoezi la utolewaji wa fomu kwa ajili ya nafasi zote za uchaguzi zilizotangazwa (ikiwemo ya Mwenyekiti) linaendekea na litafikia tamati 14/11/2018.

Amesema wale wanaomtaka Manji arejee Yanga basi ni vyema wakaenda kumchukulia fomu