TSHISHIMBI Arejea Kikosini Yanga

Baada ya kuwa nje kwa wiki kadhaa kutokana na majeruhi, kiungo wa Yanga Mcongomani Papi Tshishimbi amerejea kikosini baada ya kuanza mazoezi juzi.

Tshishimbi amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kifundo cha mguu yaliyomfanya akose michezo mitatu iliyopita ya Yanga.

Bado msimu huu haujawa mzuri kwa Tshishimbi aliyetua kwa kishindo msimu uliopita akitoka klabu ya Mbabane Swallows ambayo mwishoni mwa mwezi huu itakuja nchini kuchuana na Simba kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa.

Tshishimbi huenda akawa sehemu ya kikosi cha Yanga ambacho Jumapili Novemba 18 kitashuka uwanja wa Majaliwa wilayani Ruangwa kuikabili Namungo Fc kwenye mchezo wa kirafiki

USAJILI: Dirisha Dogo la Usajili lafunguliwa Rasmi

Jana Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kupitia Mtendaji wake Mkuu Boniface Wambura, ilithibitisha kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili leo Alhamisi Novemba 15 2018.

Wambura alisema kulingana na kalenda ya mashindano, dirisha la usajili limefunguliwa leo na litafungwa Disemba 15.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo ligi ilikuwa ikisimama kipindi chote cha usajili wa dirisha dogo, mwaka huu ligi itaendelea.

“Ni kweli kwa kalenda ya mashindano November 15 hadi December 15 linafunguliwa dirisha dogo la usajili lakini ukiangalia ratiba yetu ligi haitasimama kupisha dirisha dogo la usajili,” alisema Wambura

“Ligi kuu imesimama kupisha kalenda ya FIFA kuanzia November 12 hadi 20, baada ya hapo kutakuwa na hatua za awali za Caf Champions League na Confederation Cup, ligi itaendelea kama kawaida.

“Nadhani December 2 ligi kuu inaendelea na daraja la kwanza na daraja la pili, kwa hiyo hatutasimama tutacheza kama ilivyokuwa msimu uliopita tunacheza huku watu wanaendelea na usajili wa dirisha dogo.”

“Tunazikumbusha timu, nadhani zinajua umuhimu wa dirisha dogo, kama kuna mahali kuna upungufu warekebishe kwa sababu ndio mahali ambapo kama timu yako imecheza mechi 15 za ligi benchi la ufundi litakuwa limepata mwelekeo kwamba liimarishe kikosi wapi”

Tayari baadhi ya timu zimetambulisha wachezajiwaliowasajili. Azam Fc imemtambulisha Obrey Chirwa huku KMC ikimtambulisha Elius Maguri

Kwa upande wa Yanga Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Hussein Nyika amesema timu hiyo inaendelea na mchakato wa kukamilisha usajili wa wachezaji waliopendekezwa na kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera.

Yanga 1-1 Reha FC : Full Time

Yanga leo imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Reha Fc katika mchezo wa kirafiki uliopigwa dimba la Uhuru jijini Dar es salaam.

Bao la Yanga lilipatikana kwenye kipindi cha kwanza mfungaji akiwa kiungo Maka Edward.

Baada ya mchezo huo Yanga inatarajiwa kusafiri kwenda mkoani Lindi ambapo Jumapili Novemba 18 2018 itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Namungo Fc dimba la Majaliwa Wilayani Ruangwa

Michezo hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Yanga kabla ya kusafiri mkoani Shinyanga kuikabili Mwadui Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara

Full Time : Tanzania (U23) 0-2 Burundi (U23)

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania U23 kimeanza vibaya michuano ya kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 U23 baada ya kulazwa mabao 2-0 ugenini Burundi.

Mabao yaliyoihakikishia Burundi ushindi muhimu yalifungwa na Shaban Mabano kwa mkwaju wa penati kwenye dakika ya 59 huku bao la pili likifungwa na Cedric Mavugo‬ ‪kwenye dakika ya 79.

Vijana hao wa Tanzania sasa wanahitaji kushinda kwa zaidi ya mabao mawili kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini Novemba 20 2018 ili waweze kufuzu raundi ya pili.

Mshindi wa jumla wa raundi ya kwanza kati ya Tanzania na Burundi atachuana na Congo kwenye raundi ya pili

Simba vs Big Bullet Haji Manara Aweka wazi Viingilio

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba keshokutwa Ijumaa, Novemba 16 2018 watashuka kwenye uwanja wa Taifa kuwakabili mabingwa wenzao Nyasa Big bullets kutoka nchini Malawi katika mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo wa Kimataifa wa kirafiki unatarajiwa kuanza saa 12 jioni.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema watautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows utakaopigwa Novemba 27.

Manara ametaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni;
VIP A : 10,000/-
VIP B na C : 7,000/-
Mzunguuko : 3,000/-

Manara amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa keshokutwa ili kuiunga mkono timu yao.

Michuano ya CHALLENGE yakosa Muandaaji Mwaka Huu

Baraza la Vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limethibisha mashindano ya Kombe la Chalenji 2018, yaliyokuwa yaanze mwishoni mwa mwezi huu, hayatafanyika tena.

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amesema wameshindwa kupata nchi iliyokuwa tayari kuwa mwenyeji wa fainali hizo baada ya Kenya kujitoa.

Kenya ilipata haki za kuwa mwenyeji wa mashindano hayo baada ya kuifunga Zanzibar kwa penalti na kutwaa ubingwa huo mwaka jana.

“Kwa bahati mbaya mwaka huu hatutakuwa na mashindano ya Chalenji yanayotoa nafasi kwa timu za mataifa ya ukanda huu kushindana,” alithibisha Musonye.

“Tumejaribu kutafuta nchi nyingine, lakini muda haupo upande wetu kwa sababu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu yataanza katika hatua za awali kuanzia Novemba na hadi Desemba,” alifafanua Musonye.

Agosti baraza hilo lilipata na kiwewe baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutangaza kutokuwa na fedha kwa ajili ya kuwa wenyeji wa fainali hizo.

Hata hivyo, Musonye alithibisha kuwa Uganda watakuwa wenyeji wa mashindano ya Chalenji Cecafa U-20, yatakayofanyika kuanzia Desemba 15-23.

“Mashindano ya vijana msimu huu yatafanyika hivi karibuni tunategemea kupata ushindani wa kweli,” alisema Musonye.

Mwanaspoti

Yanga vs Reha Fc Leo Nov 14

Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga leo wanashuka kwenye uwanja wa Uhuru kuikabili Reha Fc katika mchezo wa kirafiki kwa ajili ya kukiandaa kikosi hicho.

Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga kipindi hiki ambacho ligi imesimama kupisha michuano ya Kimataifa. Jumapili iliyopita iliilaza African Lyon bao 1-0.

Ni kwa Tsh 5,000/- tu utaushuhudia mchezo huo ukiwa umekaa majukwaa ya VIP wakati kule upande wa mzunguuko ni Tsh 3,000/-

Vijana wa STARS wanacheza na Burundi

Leo Jumatano saa 10 jioni kikosi cha timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 23, kinashuka kwenye uwanja wa Prince Louis Rwagasore kuwakabili wenyeji wao Burundi katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019 kwa vijana.

Stars U23 ilisafiri na kutua Burundi jana ambapo jioni ilifanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo utakaopigwa saa kumi jioni.

Kikosi cha Stars U23 kilichokwenda Burundi kilijumuisha wachezaji 20, na viongozi wa benchi la ufundi.

Mlinda lango Ramadhani Kabwili na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kutoka klabu ya Yanga ni miongoni mwa wachezaji waliojumuishwa kwenye kikosi hicho